Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt Tedros Ghebreyesus amepongeza jitihada za Rwanda za kutokomeza ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kabla ya mwaka 2030.
Kauli ya yake inakuja baada ya taasisi ya afya RBC ya nchini humo kusema kuwa Rwanda ilikuwa imeazimia kufikia lengo la 90-70-90 katika kutokomeza ugonjwa huo, ifikapo mwaka 2027, ambayo ni miaka mitatu nyuma ya lengo lililowekwa na WHO.
Malengo hayo ni pamoja na kutoa chanjo kwa asilimia 90 ya watoto wa kike wenye umri wa miaka 15, na kuwapima asilimia 70 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 35 hadi 45.
“Tumefurahishwa na malengo yenu. Mipango hii inadhihirisha utayari kwa Rwanda kufikia malengo yake mapema, na kwamba yote haya yataweza kufanikiwa,” alisema Dkt Ghebreyesus.
Ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na mabadiliko ya mfumo wa chembechembe au seli zilizoko katika shingo ya kizazi wengine wakiita mlango wa kizazi.
Kwa mujibu wa WHO ulimwenguni kote saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ya nne kwa kuathiri wanawake, ikiwa na wagonjwa wapya 604,000 mnamo 2020.