Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula, WFP, linaonya kwamba dirisha la kuokoa maisha linafungwa huku njaa ikitanda katika maeneo yenye vita nchini Sudan.
WFP imesema katika taarifa kuwa raia wamenaswa katika mapigano makali kaskazini mwa Darfur huku msimu wa mvua uliopangwa kuanza mwezi Juni kutarajiwa kufanya njia muhimu za usafiri zisifikike.
Vita vinaendela kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces tangu Aprili 2023.
"Hali ni mbaya na inazidi kuzorota haraka. WFP kwa sasa inawafikia takriban watu milioni 2.5. Tuna uwezo wa kuongeza na kupanua usaidizi wetu, lakini kwa ajili hiyo tunahitaji pande zote kuwezesha upatikanaji - katika mstari wa mbele unaopigana, pamoja na kuvuka mpaka kutoka Chad na Sudan Kusini," alisema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau kufuatia ziara yake nchini Sudan wiki hii.
"Ni wiki chache tu zimesalia kuhifadhi chakula katika sehemu za Darfur na Kordofan kabla ya msimu wa mvua kuanza na barabara nyingi kutopitika. Wakulima pia wanahitaji kufika katika mashamba yao kwa usalama ili kupanda kabla ya mvua kunyesha,” aliongeza.
Takwimu za UN zinaashiria kuwa takriban watu milioni 5 nchini Sudan wako kwenye ukingo wa njaa huku wataalamu kutoka WFP wakionya kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka kwa kiasi kikubwa tangu tathmini ya mwisho ya mwezi Desemba 2023.
Uchambuzi wa awali wa WFP umebainisha maeneo 41 yenye njaa ambayo yanakabiliwa na hatari kubwa katika mwezi ujao, mengi zaidi.
Kati yaoni maeneo ambapo migogoro inaendelea ikiwa ni pamoja na eneo la Darfur na Kordofan na Khartoum.
Kuongezeka kwa mapigano katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini El Fasher katika siku za hivi karibuni kumesababisha idadi kubwa ya vifo vya raia na majeruhi, kuharibu hospitali pekee ya uendeshaji katika jimbo hilo, na kutatiza ufikiaji wa kibinadamu katika jiji hilo na kwengineko.
WFP imekuwa ikionya mara kwa mara kwamba Sudan inaweza kuwa janga kubwa zaidi la njaa ulimwenguni wakati mzozo huo unaingia mwaka wake wa pili.