Rais Lazarus Chakwera  alishinikizwa kumfuta kazi Waziri wa Usalama kutokana na alivyoshughulikia ajali iliyosababisha kifo cha Makamu wa Rais Saulosi Chilima/ Picha: wengine.            

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amemfuta kazi Waziri wa Ulinzi Harry Mkandawire katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri Jumatano.

Chakwera pia alimfuta kazi Naibu Waziri wa Elimu Nancy Mdooko na kuwapanga mawaziri wengine kwenye nyadhifa mpya hatua ambayo alisema katika ujumbe wake wa Mwaka Mpya kwa taifa unalenga "kutoa huduma bora zaidi kwa nchi mnamo 2025."

Awali Chakwera alipata shinikizo kubwa kutoka sekta mbalimbali za jamii kumtaka amfute kazi Mkandawire kutokana na jinsi kifo cha Makamu wa Rais Saulosi Chilima kilivyoshughulikiwa Juni 10 mwaka jana katika ajali ya ndege ya kijeshi.

Chilima na wengine nane walifariki katika ajali hiyo iliyotokea katika msitu ulioko kaskazini mwa Malawi kutokana na ukungu mnene huku jeshi likishutumiwa kwa "uzembe" katika juhudi za utafutaji na uokoaji.

George Phiri, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, alimpongeza Rais kwa uamuzi wake wa kumfuta kazi Mkandawire, na kuutaja kuwa ni “hatua katika mwelekeo sahihi.”

“Angalau Rais amedhihirisha kuwa amewasikia watu walichosema kuhusu Wizara ya Ulinzi na Waziri anayehusika. Ingawa uamuzi wa kumfukuza umechelewa kidogo, ni bora kuliko kutochukua hatua hata kidogo. Mawaziri na watumishi wengine wa umma wanapaswa kuwajibika kwa matendo yao,” Phiri alieleza Anadolu.

Lakini wataalamu wengine wamemlaumu Rais kwa kudumisha Baraza la Mawaziri lenye watu 31 wakati uchumi wa nchi hiyo 'unavuja.'

Mwanauchumi Milward Tobias aliiambia Anadolu kwamba wazo la kuendelea kuwa na Bazara la Mawaziri 31 "lilikuwa tu kutojali masaibu ya watu wa Malawi."

TRT Afrika