Shirika la kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema kuwa watu 45 wamepoteza maisha na wengine 111 hawajulikani walipo kufuatia ajali ya baharini iliyohusisha chombo kilichokuwa kimebeba wahamiaji haramu.
Tukio hilo lililotokea katika fukwe ya Obock iliyo karibu na Godoria ilihusisha boti mbili zilizokuwa zikisafirisha watu kutoka nchini Yemen.
Kwa mujibu wa walionusurika, boti ya kwanza ilibeba wahamiaji 100 huku ya pili ikiwa na 210 wote wakirejea Djibouti kutoka Yemen.
Inasemekana kuwa, wahamiaji hao walilazimishwa kushuka kushuka katikati ya bahari na manahodha wa boti hizo, kabla ya kutokea kwa ajali hiyo.
Kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), mwanamke mmoja alipoteza maisha huku mwananye mwenye miezi 4 na abiria wengine 98 wakinusurika katika ajali hiyo ya boti.
Kwa sasa, IOM inaratibu shughuli za utafutaji na uokoaji, huku hadi sasa, idadi ya watu waliokolewa ikiwa imefikia 55 na wanapokea misaada ya kisaikolojia.
"Janga hili la hivi punde ni ukumbusho mkubwa zaidi bado kuwa tuwa hitaji la dharura la kulinda na kushughulikia mahitaji ya wahamiaji kwenye Njia ya Mashariki kutoka Pembe ya Afrika hadi Yemen na Ghuba," alisema Frantz Celestin, Mkurugenzi wa Kanda wa IOM, katika maeneo ya Mashariki, Kusini na Pembe ya Afrika.
“Mamia wamepoteza maisha mwaka huu, " Celestin amesema.
Mwaka 2024, unasalia kuwa mbaya zaidi kwa matukio yenye kuhusisha vyombo vya majini katika eneo la mashariki, Yemen na pembe ya Afrika.
Tukio hili pia ni la pili kwa kusababisha vifo vingi zaidi, kufuatia ajali ya Juni 2024, ambayo iligharimu watu 196 mnamo Juni 2024.
Wahamiaji wengi hutumia njia hii kuondoka na kurejea katika nchi zao za asili, hasa Ethiopia na Somalia, wakiwa na matumaini ya kutafuta fursa za maisha bora katika nchi za Ghuba.
Hata hivyo, maelfu ya watu hao hukwama njiani wakati wengine hukabiliana na nyakati ngumu wawapo baharini.