Jeshi lilisema katika taarifa yake kwamba vikosi vya kijeshi " viliwafyatulia risasi waumini wa Kikristo / Photo: AFP

Pande zinazopigana nchini Sudan zililaumiana kuhusu shambulio dhidi ya waumini siku ya Jumapili katika mji mkuu, Khartoum, wakati wa misa katika kanisa la Coptic.

Jeshi lilisema katika taarifa yake kwamba vikosi vya kijeshi " viliwafyatulia risasi waumini wa Kikristo" katika Kanisa la Mar Girgis (St George).

Mapigano kati ya vikosi vya serikali na Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF) tangu mwezi uliopita yamesababisha vifo vya mamia na kuwaacha karibu milioni moja kuyahama makazi yao.

Mazungumzo yanayoungwa mkono na Marekani na Saudi Arabia yanaendelea katika mji wa bandari wa Jeddah lakini bado hayajafikia usitishaji mapigano.

RSF ililaumu jeshi kwa shambulio hilo ambalo "lilisababisha majeraha mabaya miongoni mwa waumini wa kanisa". Iliomba uchunguzi huru kuhusu tukio hilo.

Mashambulizi ya makombora na angani yanaendelea kushambulia maeneo ya Khartoum huku kukiwa na dalili ndogo kwamba makundi ya kijeshi yanayopigana yalikuwa tayari kurejea nyuma katika mzozo huo uliodumu kwa mwezi mzima.

Jitihada za awali za Umoja wa Mataifa na majirani wa Sudan kusitisha mzozo huo zilishindwa kushika kasi.

Makubaliano ya hivi majuzi yaliyosimamiwa na wapatanishi wa Saudia na Marekani hayafanani na mapatano bali yanatoa upitishaji salama wa misaada ya dharura ya kibinadamu na kujitolea kuwalinda raia katika mapigano hayo.

TRT Afrika