Sudan imekuwa katika vita tangu Aprili 2023 ikiwa mvutano kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces / Picha: Reuters

Umoja wa Afrika uliandaa kongamano la wanawake wa Sudan kwa nia ya kuwahusisha katika mjadala wa Sudan kurejea katika hali ya kawaida.

Sudan imekuwa katika vita tangu Aprili 2023 huku mvutano kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces ukiendelea.

"Tunaomba ushiriki wa wanawake uwe angalau asilimia 50 ya upendeleo katika ngazi zote, ikiwa ni pamoja na ngazi za kisiasa na mashinani," wamesema wanawake hao kulingana na taarifa ya Umoja wa Afrika.

"Kuna haja ya kuhakikisha kuwa haki za wanawake zinawekwa katika ajenda ya mazungumzo, katika vifungu vya makubaliano yoyote ya amani, na kwamba wanawake pia wahusishwe katika kutia saini mikataba ya amani," wameongezea.

Pande zinazopigana zimeshindwa kutekeleza masharti ya makubaliano yaliyotiwa saini mjini Jeddah tarehe 11 Mei 2023 yanayohusiana na ahadi za kulinda raia.

"Tunasikitishwa sana na vita vinavyoendelea kote nchini Sudan, ambavyo vina athari mbaya kwa watu wa Sudan haswa, wanawake na wasichana na vikundi vilivyo hatarini, pamoja na uharibifu wa miundombinu ya kijamii, pamoja na kilimo, afya na huduma nyengine," wamenukuliwa wanawake hao wakisema, kwa mujibu wa Umoja wa Afrika.

Wanawake wa Sudan waliokuwa katika mkutano huo pia wametaka wanawake wahusishwe katika ufuatiliaji na utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, vita nchini humo vimelazimisha zaidi ya watu milioni 10 kukimbia makwao, wengi wakikimbilia nchi jirani za Sudan Kusini, Chad na Ethiopia.

udan

TRT Afrika