Raia wa Mali wanapiga kura, Jumapili katika kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba ambayo serikali ya kijeshi inayotawala na mamlaka ya kikanda zinasema itafungua njia ya kuandaa uchaguzi na kurejea kwa utawala wa kiraia.
Mali ilishuhudia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2020 na 2021.
Jeshi limeahidi kuelekea katika demokrasia chini ya shinikizo la jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS.
Baadhi ya mabadiliko katika katiba iliyoandaliwa na kamati hiyo yana utata, huku wanaoiunga mkono wakisema yataimarisha taasisi tete za kisiasa lakini wapinzani wanasema yangempa rais mamlaka makubwa.
Mashirika ya kikanda na Umoja wa Mataifa wanaona kura ya maoni yenyewe kama mtihani muhimu kwa wanajeshi wanaoongoza sasa, kuona kama kweli wataheshimu mchakato wa kidemokrasia wa nchi nzima, hasa wakati ambapo wanamgambo wa Kiislamu wanazidisha mashambulizi.
Mali mpya
"Kwa mradi huu, tunatumai kutarudishia serikali yetu ya wananchi mamlaka yake, na kuaminiana tena kati ya taasisi na raia," rais wa mpito Assimi Goita alisema katika hotuba ya televisheni siku ya Ijumaa.
"Sasa ni wakati wa kuthibitisha kujitolea kwetu kwa Mali mpya," aliongeza, akiwa amevalia sare za jeshi.
Raia wapatao milioni 8.4 wanatarajiwa kupiga kura ya "ndiyo" au "hapana" katika rasimu ya katiba katika jaribio la kwanza la uchaguzi kwa kiongozi Kanali Assimi Goita, 40, ambaye ameapa kuiongoza nchi hiyo na kuirejesha katika utawala wa kiraia katika uchaguzi wa 2024.
Lakini Mali ina historia ya idadi ndogo ya watu kujihusisha katika uchaguzi, na wachambuzi wengi wanasema wakati huu huenda isiwe tofauti.
Nchi hiyo yenye watu milioni 21 imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa na ukosefu wa usalama huku makundi yenye silaha yakifanya mashambulizi katika maeneo ya kati na kaskazini.
Kutokana na matatizo ya kiusalama, kura hiyo haitafanyika katika baadhi ya maeneo ya nchi, ikiwa ni pamoja na Kidal, ngome ya waasi wa zamani kaskazini mwa nchi hiyo.
Matokeo ya muda yanatarajiwa ndani ya saa 72 baada ya kufungwa shughuli ya kupiga kura.
Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika Februari 2024.