Jumatatu ni siku ya mwisho ya zoezi la Ushiriki wa Umma kwenye Muswada wa fedha 2024.
Kamati ya Idara ya Fedha na Mipango ya Kitaifa nchini Kenya inaendesha mkutano wa hadhara kuhusu muswada huo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi.
Muswada wa Fedha 2024 wa mapendekezo ya kuongeza ushuru umezua mjadala mkubwa nchini humo huku wengi wa wananchi wakiukataa.
Wengi wamedai kuwa mapendekezo hayo iwapo yataingizwa kwenye muswada basi yataongeza gharama ya maisha.
Maoni ya wananchi
Zaidi ya wadau 600 waliofika mbele ya kamati hiyo wametoa maoni yao kupinga muswada huo.
“Pendekezo la kutoza VAT kwa mkate litaathiri vibaya shule. Ikiwa VAT itawekwa, bei ya mkate itaongezeka kwa takriban Kshs. 10-12, ambayo tafsiri yake ni takriban Kshs. 3,000 kwa mwezi,” Pamphil Omondi, mwanaharakati wa elimu amesema katika mkutano huo.
Hellen Nafula amezungumza kuunga mkono masharti ya Kifungu ambacho kinalenga kuongeza ushuru wa sigara, kutokana na mchango wao katika kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani.
Mwananchi mwengine John Momanyi anayewakilisha kampuni ya chakula cha wanyama, Sigma Feeds ameunga mkono pendekezo linalotaka kutojumuisha mayai yaliyorutubishwa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo yanakidhi Kanuni au Asili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naye Benson Amburi anayewakilisha Chama cha Wastaafu nchini Kenya, alipokuwa akitoa mawasilisho yake kuhusu Muswada wa fedha 2024, ameitaka Kamati kuzingatia kupanua wigo wa ushuru ili kuwanasa Wakenya ambao kwa sasa hawako kwenye mabano ya ushuru.
Uchunguzi uliofanywa na kampuni ya uchunguzi ya Infotrak ukisema Wakenya 4 kati ya 5 wanapinga baadhi ya mapendekezo makuu ya ushuru katika Muswada huo unaolenga kuongeza Ksh. bilioni 300.
Shirika hilo lilihoji watu 1,700 katika kaunti 47 za Kenya.
Kulingana na kura ya maoni iliyofanywa na kampuni hiyo kati ya Mei 25 na Mei 29 2024, asilimia 77 ya Wakenya walisema Muswada wa Fedha wa 2024 hautakuwa na matokeo chanya kwa uchumi huku asilimia 13 ya waliohojiwa wakisema kuwa utakuwa na athari chanya.
Asilimia 87 ya Wakenya waliohojiwa wanapinga kuanzishwa kwa asilimia 16 ya VAT kwa mkate huku asilimia 86 wakipinga kuanzishwa kwa huduma za VAT kwenye miamala ya kifedha kama vile M-PESA.
Ushuru mwingine katika Mswada wa Fedha ambao Wakenya walikataa ni pamoja na ushuru wa utangulizi wa asilimia 2.5 ya thamani ya magari (asilimia 81), ushuru wa ziada kwa bidhaa zisizo rafiki (asilimia 83) na pendekezo la kusamehe ufichuzi wa bidhaa kibinafsi, taarifa na vidhibiti taarifa kwa mtu wa ushuru (asilimia 83).
Ushiriki wa umma una umuhimu gani?
Kushirikisha umma ni mahitaji ya katika kabla ya muswada wowote kupitishwa kuwa sheria ikiangaliwa kama mojawapo ya nguzo za demokrasia, ushiriki wa umma kuhusisha wananchi na wale wanaohusika kwa njia moja au nyengine na masuala amabayo yanapendekezwa katika muswada.
Ushiriki wa umma na shinikizo mnamo 2023 uliilazimisha Bunge la Kenya kupunguza lengo la Muswada wa Fedha wa mwaka 2023 kutoka dola bilioni 2.1 hadi dola bilioni 1.6.
Kupuuza maoni ya wananchi pia kunapoteza rasilimali za serikali huku wadau wengi wakikimbilia mahakamani kusitisha utekelezaji wa vitendo mbalimbali vya sheria mpya.
Katika kesi ya Muswada wa Fedha wa 2023, Seneta wa Busia, Okiya Omtatah na Chama cha Wanasheria wa Kenya walienda kortini wakitaka kusitishwa kwa utekelezaji wa Sheria hiyo wakitaja sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupuuza maoni ya umma.