Zaidi ya watu 35 wamekufa katika "shambulio la kigaidi" katika shule moja magharibi mwa Uganda, msemaji wa jeshi la Uganda alisema Jumamosi.
Wanamgambo wa Allied Democratic Forces, (ADF), wanaoungwa mkono na Daesh wamelaumiwa kwa shambilio hilo.
"Hadi sasa maiti 37 zimepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti, hospitali ya Bwera, huku watu wanane wakilazwa wakiwa na majeraha,'' amesema msemaji wa jeshi Brigadia Jenerali Felix Kulaije. '' UPDF imeanzisha msako wa wanamgambo hao kwa lengo la kuwaokoa takriban wanafunzi 6 waliotekwa nyara.'' Ameongeza Kulaije.
Duru za jeshi zinassema kuwa wanafunzi hao walitumika kubeba chakula kilichoporwa kutoka shuleni kuelekea mbuga ya wanyama ya Virunga.
ADF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu shambulio hilo.
Polisi haijathibitisha ni wangapi kati ya waliofariki walikuwa watoto wa shule.
Je, waaasi wa Allied Democratic Forces (ADF) ni nani?
Kikundi cha Allied Democratic Forces (ADF) ni kundi lenye silaha wananaopatikana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kikundi hiki kilundwa mnamo 1995, kupigana dhidi ya utawala wa rais wa Uganda Yoweri Museveni. Kilipoundwa kilikuwa na muungano wa vikosi vya waasi vikiwemo, Uganda Muslim Liberation Army na National Army for the Liberation of Uganda (NALU).
Tangu wakati huo wamekuwa wakishutumiwa kufanya mashambulio na mauaji ya maelfu ya raia.
Wapiganaji wa ADF kimsingi wanatoka Uganda na DRC, huku wengine wakiripotiwa kutoka mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Tangu mwaka 2019, baadhi ya mashambulizi ya ADF mashariki mwa DRC yamedaiwa kufanywa na Daesh kwa jina lingine kundi la 'Islamic State', ambalo linawataja wapiganaji kuwa na uhusiano na kundi lao.
Uganda imelaumu ADF kwa mashambulizi mabaya ya kujitoa mhanga katika mji mkuu, Kampala. Kundi hilo lenye silaha pia limehusishwa na mashambulizi Mashariki mwa DRC.