Wanajeshi wa Mali wameanzisha mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa kigaidi katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, karibu na mpaka na Algeria.
"Lengo la operesheni hii ni kurejesha udhibiti wa Tinzaouatene, mji wa mwisho wa mpaka wa Algeria ambao bado uko chini ya uvamizi wa magaidi," Serikali ya Mali ilisema Jumatatu katika taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa X na kituo cha habari cha Muungano wa Nchi za Sahel (AES).
AES inajumuisha Mali, Burkina Faso, na Niger, ambazo zote ziko chini ya utawala wa kijeshi.
"Awamu hii mpya ya mapambano dhidi ya ugaidi nchini Mali inaashiria kuimarika kwa juhudi za kulinda maeneo ya mpaka," iliongeza taarifa hiyo.
Mapambano dhidi ya waasi Mali
Sawa na majirani zake wa Sahel Burkina Faso na Niger, Mali imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya waasi, ambayo yamegharimu maisha ya maelfu ya watu, na hata idadi kubwa zaidi ya watu kuyahama makazi yao.
Mashambulizi hayo ya kaskazini yanajiri wiki mbili baada ya kundi la wanamgambo la JNIM kudai kuhusika na shambulio kubwa katika mji mkuu wa Mali, Bamako na kusababisha vifo vya takriban watu 77.
Mali, Burkina Faso na Niger, ambazo zimetangaza kuondoka katika jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS, zimeimarisha mapambano yao dhidi ya waasi, zikisema moja ya malengo makuu ya Muungano wa Nchi za Sahel ni kuyalinda mataifa hayo matatu dhidi ya ugaidi.
Mali pia imeweza kurudisha miji muhimu - ikiwa ni pamoja na Kidal kaskazini mashariki - ambayo hapo awali ilikuwa chini ya udhibiti wa watu wanaotaka kujitenga wa Tuareg.