Wanajeshi wawili wa Afrika Kusini wameripotiwa kuuawa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya bomu kushambulia kambi yao Picha:  SANDF/X

Wanajeshi wawili wa Afrika Kusini wameripotiwa kuuawa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya bomu kushambulia kambi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

"Vikosi vya ulinzi vya Kitaifa vya Afrika Kusini vinathibitisha kwamba mnamo tarehe 14 Februari 2024, mwendo wa saa saba mchana, bomu lilirushwa ndani ya kambi moja ya kijeshi ya Afrika Kusini na kusababisha vifo na majeraha," taarifa kutoka Jeshi la Taifa la Afrika Kusini limesema.

Mapema wiki hii, rais Cyril Ramaphosa alitangaza kutumwa kwa wanajeshi 2,900 nchini DRC kama sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) yenye nia ya kupambana na makundi yenye silaha. Wanajeshi hao wataendelea kupelekwa nchi DRC hadi Disemba 15, 2024.

"Kutokana na shambulio hilo, maafisa wawili wa Jeshi la Tafa la Afrika Kusini walikufa na wengine watatu kujeruhiwa. Walipelekwa hospitali ya karibu ya Goma kwa ajili ya matibabu," taarifa hiyo imeongezea.

Jeshi la Afrika Kusini limesema bado hakuna taarifa za kutosha kuhusu mashambulizi haya kwa sasa, wakati uchunguzi ukiendelea.

Taarifa zaidi kuhusu mauaji ya wanajeshi hao wa DRC zinategemea kuendelea kutoka.

TRT Afrika