Wanaharakati watatu wa Kenya wanaodaiwa kutekwa nyara mwezi Agosti 2024 kufuatia maandamano ya kuipinga serikali wameachiliwa. Hii ni kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Wanaume hao wanadaiwa kutekwa na vikosi vya usalama kwa wiki kadhaa.
Bob Njagi, Aslam Longton na kaka yake Jamil Longton waliachiliwa nje ya jiji la Nairobi siku ya Alhamisi, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu lilisema.
"Washirika wetu wamethibitisha kuachiliwa kwao," Cornelius Oduor, wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya aliiambia AFP.
"Picha zinaonyesha wazi kwamba walikuwa katika dhiki... inaashiria ukweli kwamba wamekuwa utumwani."
Kesi hiyo imezua ghadhabu kubwa na kusababisha uchunguzi kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vya usalama vya Kenya.
Kutekwa nyara kwao kulikuja huku kukiwa na wimbi la maandamano dhidi ya serikali ya Kenya mwezi Juni.
Zaidi ya watu 60 walipoteza maisha wakati wa maandamano hayo, na kusababisha Mkuu wa Polisi kujiuzulu. Kesi hiyo inaangazia changamoto zinazoendelea zinazowakabili wanaharakati na mashirika ya kijamii nchini Kenya.
Jela kwa Naibu Mkuu wa Polisi
Naibu Inspekta Jenerali wa polisi wa Kenya alijipata mashakani baada ya kuibuka kwa kesi hii na kushindwa kuitikia wito wa mahakama kwa mara kadhaa ili kujibu tuhuma za kupotea kwa watu hao.
Gilbert Masengeli alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela Septemba 13, 2024.
Hii ni baada ya kiongozi huyo wa polisi kudharau wito wa mahakama kwa mara saba mfululizo.
"Bwana Masengeli anaamriwa kujisalimisha kwa Kamishna Jenerali wa Magereza ili kuhakikisha kuwa anawekwa gerezani kutumikia kifungo chake," alisema Jaji Lawrence Mugambi.
Masengeli alitarajiwa kufika mahakamani kulingana na amri ya Jaji Lawrence Mugambi ndani ya siku saba kutoka wakati huo.
Hata hivyo 19 Septemba 2024, Jaji Chacha Mwita wa Mahakama ya juu alikataa ombi lake la kufika mbele ya Jaji Lawrence Mugambi kuomba msamaha.
Licha ya marufuku ya kufika mahakamani, mapema hii leo alijitokeza.