Serikali ya Kenya imesema kuwa familia za watu walioathirika katika mauaji ya ibada ya njaa Pwani ya Kenya mwaka uliopita wataanza kupokea mabaki ya jamaa zao.
Kuanzia Machi 26, 2026 familia za watu 34 ambao miili yao ilifukuliwa na kutambuliwa kutoka eneo la kaburi la watu wengi la Shakahola katika kaunti ya Kilifi wataanza kupokea mabaki yao.
Hii ni kulingana na mtaalamu wa serikali wa patholojia Dkt Johansen Oduor aliyewapa waandishi wa habari ripoti hii akiwa hospitali ya Malindi.
Oduor amesema kuwa Serikali itatoa huduma za ushauri nasaha kwa familia zilizoathiriwa kabla ya kuwakabidhi miili hiyo.
Ameongezea kuwa watu waliotoa sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba DNA lazima wawepo wakati wa mchakato wa kukusanya miili.
Wakati huo huo, serikali imesema itazizika maiti ambazo hazijatambuliwa na kudaiwa kwa kufuata sheria.
Zoezi la ufukuaji wa miili ya watu hao kutoka katika makaburi 35 yaliyotambuliwa huko Shakahola utaendelea tena.
Mwezi Februari mwaka huu, mahakama nchini Kenya ilimshtaki kiongozi wa kundi la waumini wa njaa na wengine wanaoshukiwa kuhusika na mauaji kutokana na vifo vya takriban watu 200 katika msitu wa Shakahola, Pwani ya Kenya.
Tukio hilo lilitokea mwaka 2022.
Kiongozi wa ibada hii ni Paul Nthenge Mackenzie, ambaye tayari amefunguliwa mashtaka ya ugaidi, kuua bila kukusudia na vile vile kutesa watoto na ukatili, anadaiwa kuchochea mamia ya wafuasi wake kufa kwa njaa kwa madai kuwa "watakutana na Yesu."
Mackenzie na washukiwa wengine 29 walikana mashtaka 191 ya mauaji, kulingana na hati za mahakama.