Kundi la wanaharakati nchini Morocco limeitaka serikali kuzuia meli ya mizigo, Vertom Odette, inayoshukiwa kusafirisha silaha za India kwenda Israeli kupita katika eneo lake la maji.
Kulingana na kundi hilo la Morocco Front for Supporting Palestine and Opposing Normalization," meli hiyo ya kibiashara inasafiri chini ya bendera ya Luxemburg, iliondoka India Aprili 18 na inatazamiwa kuwasili katika bandari ya Uhispania ya Cartagena siku ya Jumatano. Chombo cha habari cha National News kiliripoti Jumanne.
Ili kuingia Mediterania, meli zinazosafiri mashariki kutoka Atlantiki lazima zipitie Mlango-Bahari wa Gibraltar, unaotenganisha Hispania na Morocco.
Katika barua kwa serikali, kundi hilo lilionyesha wasiwasi kuwa meli hiyo ilikuwa ikisafirisha shehena ya silaha zinazopelekwa Israeli, na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka ili kuzuia kile ilichokitaja kuhusika kwa Morocco "katika uhalifu wa kivita."
Iliongeza: "Uamuzi wa hivi majuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ulisema kuwa taifa hilo linaloikalia Palestina kwa mabavu linapaswa kuwa makini kutofanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Uamuzi huu unaifanya kila serikali inayoipatia Israeli silaha kuwa katika hatari ya kutuhumiwa kuhusika na mauaji hayo ya kimbari."
Vita vya mauaji ya kimbari
Mamia ya watu pia wamechapisha mtandaoni kutoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua zote zinazohitajika kuzuia meli ya Vertom Odette kuingia kwenye maji ya Morocco na kuhakikisha kwamba haifiki Israeli.
Nchi nyingi duniani zilishuhudia maandamano ya kupinga vita vya Israeli dhidi ya Gaza.
Israeli imeendeleza mashambulizi yake ya kikatili huko Gaza tangu Oktoba, 2023 licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano.
Tel Aviv imewaua zaidi ya Wapalestina 36,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine karibu 83,000, kulingana na mamlaka ya afya huko Gaza.
Takriban miezi nane ya vita vya Israeli, maeneo makubwa ya Gaza yamekuwa magofu huku kukiwa na kizuizi cha chakula, maji safi na dawa.
Israeli inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo katika uamuzi wake wa hivi majuzi imeiamuru Tel Aviv kusitisha mara moja operesheni yake katika mji wa kusini wa Rafah, ambako zaidi ya Wapalestina milioni moja walikuwa wamekimbilia kutafuta hifadhi.
Uhusiano wa India na Israeli
India ndiyo mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha za Israeli, ambazo baadhi yake hutumika katika maeneo yenye utata kati ya India na Kashmir.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, India imeripotiwa kuingiza dola bilioni 2.9 za vifaa vya kijeshi kutoka Israeli. Mauzo hayo ni pamoja na ndege zisizo na rubani, makombora, rada na mifumo mengine ya upelelezi. India na Israeli zilianza kuwa na uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1992 lakini mauzo ya silaha kati ya Tel Aviv na New Delhi yalianza miaka ya 1960.
Silaha za Israeli ziliisaidia India katika vita dhidi ya China na Pakistan. Elbit Systems, moja ya kampuni kubwa zaidi ya kijeshi ya Israeli, mnamo 2018 ilikubali kufanya kazi na kampuni ya India ya Adani Group kutengeneza ndege zisizo na rubani za Hermes 900 katika kituo kilicho kusini mwa India, ambazo zinasafirishwa baadae kurudi Israeli.
Baadhi ya ndege hizo za mauaji zimeripotiwa kupelekwa Israeli kutoka India na kutumika katika uvamizi wa Gaza.