Rwanda imetoa maelekezo ya kuwataka walimu wa nchi hiyo kuongeza ustadi katika lugha ya Kiingereza.
Agizo jipya la Waziri Mkuu linamtaka mwalimu aliyemaliza muda wa majaribio kufanya mtihani wa Kiingereza kila baada ya miaka mitatu, na iwapo atafeli mtihani mara mbili mfululizo basi atafukuzwa kazi.
Agizo hilo lilichapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali mnamo Novemba 14.
"Tathmini zilizofanywa katika maeneo mbalimbali zimeonyesha kuwa ujuzi wa walimu wengi wa Kiingereza uko chini ya kiwango kinachotarajiwa ili kufundisha kwa ufanisi, jambo ambalo huathiri matokeo ya wanafunzi," Waziri wa Elimu Joseph Nsengimana alisema.
Rwanda iliitambua rasmi lugha ya Kiingereza kama lugha ya mafunzo mwaka 2009. Serikali ilisema kuwa lugha ya Kiingereza inahitajika kama zana ya mawasiliano na vile vile ya ukuzaji.
Tangu mwaka 1996 lugha zote tatu rasmi - Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza zimetumika kufundishia elimu.
Hatua hiyo, ililenga kuimarisha uhusiano wa Rwanda na majirani zake wa Afrika mashariki wanaozungumza Kiingereza, zikiwemo Uganda, Kenya na Tanzania, ambao wanafanya biashara na Rwanda. Mwaka 2009, Kigali iliomba kujiunga na Jumuiya ya Madola ingawa nchi hiyo haikuwahi kuwa koloni la Uingereza, nchi ya pili baada ya Msumbiji. Ombi lao lilikubaliwa mnamo Novemba 2009 na kuwa mwanachama wa 54 wa jumuia hiyo.
Wizara ya Elimu ilisema kuwa itawasaidia wanafunzi kupata faida sawa katika soko la ajira la Afrika Mashariki kama ilivyo kwa wanachama wengine.
Kuhusu msaada unaohitajika kwa walimu, Waziri wa Elimu alisema kuwa serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na wadau wake wakuu inatekeleza mpango wa mafunzo yenye lengo la kuboresha ujuzi wa walimu wa Kiingereza.
Walimu watasaidiwa kupitia mpango za kujiendeleza kitaaluma, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya mtandaoni ya haraka, kozi za lugha zinazolengwa, fursa za ushauri, mitandao ya usaidizi kutoka kwa wenzao na uzoefu wa lugha ya ndani.