Vijana wanaoongoza kampeni ya kupinga Muswada wa Fedha 2024 wanataka serikali iutupilie mbali kabisa / Picha: Wengine 

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kwa wiki ya pili sasa vijana nchini Kenya wanaendelea kuongoza maandamano yanayopinga Muswada wa Fedha 2024 ambao serikali ya Rais William Ruto unauona kama chanzo cha mapato zaidi.

Rais William Ruto amesema serikali yake iko tayari kufanya mazungumzo na vijana wanaoandamana ili kujadili wanachopinga katika muswada huo tata kwa lengo la kupata suluhu.

Hata hivyo, swali lililoibuka hapa ni, je, Rais Ruto atafanya mazungumzo hayo na nani, kwa sababu maandamano yanayoendelea hayajaratibiwa na kiongozi yoyote. Ni mandamano yaliyopangwa kupitia mitandao ya kijamii na kujumuisha vijana wa kada tofauti kutoka maeneo mbalimbali ya nchini.

Lakini kwa nini kuna tashwishi sasa?

Kila mwaka, serikali hupendekeza muswada wa fedha wenye nia ya kutoa mapendekeo ya jinsi ya kukusanya fedha ambazo Wizara ya Fedha hupendekeza katika bajeti.

Wiki iliyopita muswada huo ulipita awamu ya kwanza bungeni baada ya wabunge 204 kupiga kura ya kuuunga mkono/ Picha: AFP 

Muswada wa Fedha 2024 unataka kuongeza mapato kwa zaidi ya dola bilioni 2.3, kiasi kikubwa zaidi cha mapato ya ziada katika historia ya Miswada ya Fedha ya Kenya.

Hii inawakilisha ongezeko la 43%, ikilinganishwa na Muswada wa Fedha wa 2023, ambao ulitaka kuongeza dola bilioni 1.6. na Serikali imependekeza kuongeza ushuru tofauti ili kufikia malengo haya.

Lakini vijana wanaoongoza kampeni ya kupinga muswada huu wanataka serikali iutupilie mbali kabisa.

Rais wa Kenya William Ruto amesema serikali yake iko tayari kuongea na vijana wanaopinga Muswada wa Fedha 2024/ Picha kutoka Rigathi Gachagua, X

Kutokana na shinikizo la wananchi, serikali tayari imejaribu kuwashawishi wananchi kwa kufanya baadhi ya marekebisho ikiwemo kuondoa mapendekezo ya asilimia 16 ya VAT kwenye mkate, usafirishaji wa sukari, huduma za kifedha, miamala ya fedha za kigeni pamoja na asilimia 2.5 ya Ushuru wa Magari.

Pia zaidi imetupilia mbali ongezeko la ada za uhamisho wa pesa kupitia simu, na Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya mboga.

Hata hivyo, hatua hiyo, bado haijaweza kutuliza hasira za wananchi.

Baadhi ya waandamaji wanaopinga Muswada wa Fedha 2024 jijini Nairobi, Kenya: Picha Reuters 

Vijana wanasema hawataki marekebisho, bali wanataka muswada wote utupiliwe mbali. Muswada huu ukikataliwa serikali inadai kuwa utaleta pengo la zaidi ya dola bilioni 1.5 katika mapato na hii itapunguza rasilimali zinazofaa kwenda katika lishe mashuleni, fedha kwa wasiojiweza na masuala mengine.

Wiki iliyopita, muswada huo ulipita awamu ya kwanza bungeni baada ya wabunge 204 kupiga kura ya kuuunga mkono.

Wiki hii muswada unarudi bungeni kuingia katika awamu ya kamati au 'committee stage' ambayo majadiliano yanatarajiwa kufanya mabadiliko kadhaa katika mapendekezo ya muswada.

Kenya inashuhudia mvutano mkubwa kwa sasa, huku serikali na wananchi wakivutana kuhusu muswada huo tata/ Picha: AFP 

Baadaye utaingia katika awamu ya kusomwa kwa mara ya tatu au 'third reading.' Ukipita hapo, basi utapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kuidhinishwa kuwa sheria.

Wabunge wakiamua wanaweza kuusimamisha muswada huu katika awamu hii ya kamati na kuufanya usiende kusomwa kwa mara ya tatu na hatimae kufika mezani kwa rais.

Na hata ukipita awamu ya kamati bado wanaweza kuusimamisha usipite awamu ya usomaji wa tatu.

Hili likifanyika, basi serikali itahitajika kuuleta tena muswada huo bungeni baada ya miezi sita na mapendekeo mapya ya mabadiliko.

Muswada huu kutopitishwa haimaanishi kuwa serikali haitapata mapato. La itandelea kukusanya ushuru kulingana na muswada wa fedha wa mwaka uliopita.

Kenya inashuhudia mvutano mkubwa kwa sasa, huku serikali na wananchi wakivutana kuhusu muswada huo tata.

TRT Afrika