Wabunge wawili wa  chama cha Conservative wamejiuzulu wakipinga mswada wa kuhamisha waomba hifadhi Rwanda / Picha: AFP

Katika pigo kubwa kwa serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, manaibu wenyekiti wawili wa chama cha Conservative, Lee Anderson na Brendan Clarke-Smith, pamoja na katibu binafsi wa bunge Jane Stevenson wamejiuzulu wakipinga mswada wake mkuu wa Rwanda.

Sheria hiyo yenye utata inalenga kufufua mpango wa serikali wa kutuma baadhi ya waomba hifadhi nchini Rwanda kama sehemu ya juhudi za kuwazuia watu kuvuka na kuingia Uingereza kwa kutumia boti ndogo.

Hatua hiyo inajiri kama sehemu ya uasi mpana wa takriban wabunge 60 ambao wanaunga mkono marekebisho yanayolenga kuimarisha sheria ya uhamiaji iliyopendekezwa na serikali.

Licha ya kujiuzulu na kuongezeka kwa upinzani ndani ya chama, Downing Street inasalia na imani kuwa mswada wa Rwanda utapitishwa katika kura muhimu iliyopangwa kufanyika Jumatano.

Lakini kutokana na ripoti iliyopendekeza kuwa angalau wabunge 30 wanaweza kujiunga na upinzani katika kupiga kura dhidi ya mswada huo, kuna uwezekano kwamba unaweza kushindwa.

Mkataba mpya

Mwezi Disemba mwaka uliopita Uingereza na Rwanda zilitia saini mkataba mapya katika jitihada za kufufua pendekezo linaloonekana kuwa na utata la Uingereza la kuwahamisha wahamiaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambalo lilipingwa na mahakama ya Uingereza.

Makubaliano hayo, ambayo, kulingana na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ni muhimu kutimiza ahadi yake ya kukata uhamiaji usio wa kawaida kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka ujao, ulisainiwa mjini Kigali.

Sheria ya hapo awali ilikuwa inasema kuwa watu watakaoingia Uingereza kinyume cha sheria watarejeshwa katika nchi yao au kuhamishiwa Rwanda.

Rwanda itapokea takriban dola milioni 177 ili kupokea wahamiaji kutoka Uingereza.

Wahamiaji wa kwanza walipaswa kutumwa Rwanda mwezi Juni mwaka jana lakini walizuiwa wakiwa kwenye ndege dakika ya mwisho baada ya jaji katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kutoa amri ya katazo.

Tangu wakati huo, kesi zao - na uhalali mpana wa sera - zimekwama katika mahakama.

Mwezi Juni 2023 mahakama ya rufaa ya Uingereza ilitoa uamuzi kwamba mpango wa serikali ya Uingereza wa kuwapeleka wakimbizi waomba hifadhi nchini Rwanda ni batili kisheria.

Walisema kuwa serikali ya Uingereza haiwezi kuhakikisha kuwa wakimbizi waliotumwa Rwanda hawatarejeshwa katika nchi wanayokimbia.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak yuko chini ya shinikizo kubwa la kupunguza uhamiaji, ambao uligonga rekodi ya watu 745,000 mwaka jana, na kumaliza mtiririko wa wanaotafuta hifadhi ambao hulipa wasafirishaji wa watu kwa njia zao hatari za kuvuka, mara nyingi katika boti zilizojaa, na kutofaa kwa safari za baharini.

Mpango huo wa uhamiaji wa Rwanda ulitangazwa na Waziri Mkuu wa zamani Boris Johnson 2022.

TRT Afrika