Waasi wa M23 wanazidi kusonga mbele mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kusonga huko kunatupilia mbali mwito wa kusitishwa katika mji wa Goma.
Waasi hao wamekaribia eneo la Katana eneo la Kabare katika jimbo la mashariki la Kivu Kusini nchini DRC.
Waasi waliendelea kusonga mbele baada ya kukiuka safu ya ulinzi ya vikosi vya Kongo huko Ihusi, iliyoko katika eneo la Kalehe, Jumatano mwishoni, kulingana na Radio Okapi ya eneo hilo.
Mapigano kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa Kongo yalianza tena Jumanne kwenye eneo la Lubero katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kufuatia mashambulizi ya waasi dhidi ya vikosi vya jeshi la Congo.
Hapo awali, M23 ilitangaza kusitisha mapigano kwa upande mmoja baada ya kupambana na jeshi la Congo kuudhibiti mji wa Goma.
Licha ya kusitishwa kwa mapigano kwa upande mmoja, waasi wa M23 waliuteka mji wa Nyabibwe wiki iliyopita.
Hayo yakijiri serikali ya Congo imetoa wito wa kuitishwa kwa mkutano wa dharura wa wakuu wa ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kama ilivyoamuliwa katika mkutano wa jumuiya hizo mbili.
Viongozi wa EAC na SADC waliwaagiza wakuu wa ulinzi kutoka kambi zote mbili kukutana ndani ya siku tano ili kusaidia katika "kutekeleza usitishaji vita wa mara moja, usio na masharti na usitishaji wa uhasama," katika mkutano huo wa pamoja Jumamosi.
Ikiashira ahadi yake ya maazimio ya mkutano wa kilele wa pamoja, Kinshasa ilizitaka jumuiya za kikanda kuitisha mkutano wa dharura ili kutathmini hali na kujibu "kitendo hiki kipya cha uchokozi."
Ikilaani "ukiukaji" wa usitishaji mapigano wa Rwanda na "washirika wao wa M23," Congo iliomba kulaaniwa "kwa kauli moja" pamoja na vikwazo vya EAC na SADC dhidi ya Rwanda.
Waasi wa M23 sasa wanadai kuudhibiti Goma na wametangaza utawala wao katika mji huo.
Tangu Januari 26, zaidi ya watu 3,000 wameuawa, 2,880 wamejeruhiwa, na zaidi ya 500,000 wamekimbia makazi yao, ikiwa pamoja na watu milioni 6.4 ambao tayari wamekimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Takriban wanajeshi 20 wa kulinda amani wakiwemo 14 kutoka Afrika Kusini wameuawa wakati wa mapigano kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa Congo.
Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na kutuma vikosi vyake mashariki mwa Congo wakati mashambulizi ya hivi punde yalipoanza, huku Kigali ikikanusha mara kwa mara madai kwamba inawaunga mkono waasi.