Kundi la waasi la M23 limeuteka Rubaya, mji wa uchimbaji madini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) unaojulikana kwa kutengeneza madini muhimu yanayotumika katika simu za kisasa, kundi hilo lilisema katika taarifa yake.
Msemaji wa kundi la waasi la M23 alisema siku ya Alhamisi kwamba mji huo "ulikombolewa."
Jeshi la Kongo lilikataa kuzungumzia hali hiyo.
Mji wa Rubaya katika wilaya ya Masisi una akiba ya tantalamu, ambayo imetolewa kutoka kwa coltan, ambayo ni sehemu muhimu katika utengenezaji wa simu mahiri.
Ni miongoni mwa madini ambayo yalitajwa mapema mwezi huu katika barua kutoka kwa serikali ya DRC ikihoji Apple kuhusu ujuzi wa kampuni ya teknolojia ya "madini ya damu" yanayosafirishwa katika mnyororo wake wa usambazaji.
Mzozo huo uliodumu kwa miongo kadhaa mashariki mwa DRC umesababisha moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani, huku takriban makundi 120 yenye silaha yakipigania udhibiti wa eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini karibu na mpaka na Rwanda.
Makundi mengi yanatuhumiwa kutekeleza mauaji ya halaiki, ubakaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu. Ghasia hizo zimesababisha watu wapatao milioni 7 kuyahama makazi yao, wengi wao hawakuwa uwezo wa kupata misaada.
"Kuanguka kwa Rubaya ni mfano halisi wa uporaji huu wa kimfumo," Ernest Singoma, mwanaharakati wa mashirika ya kiraia huko Goma, aliliambia shirika la habari la AP.
Kumekuwa na ongezeko la mapigano katika miezi ya hivi karibuni kati ya waasi wa M23 na vikosi vya jeshi la DRC, na inakuja wakati Umoja wa Mataifa ukipanga kuwaondoa askari wa kulinda amani katika eneo hilo ifikapo mwisho wa mwaka.
John Banyene, mwanaharakati wa mashirika ya kiraia, aliiambia AP kwamba waasi walikuwa wanasonga mbele kuelekea mji wa Goma, ambao ni mji mkubwa wa mashariki mwa DRC na mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
"Njia zote za usambazaji hadi mjini zimefungwa," alisema Banyene."
'M23 na unyonyaji wa rasilimali za madini'
Rais wa DRC Felix Tshisekedi anadai Rwanda inaivuruga nchi yake kwa kuwaunga mkono waasi wa M23. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, pia wameishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi. Rwanda inakanusha madai hayo.
Mapema wiki hii, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitoa wito kwa nchi jirani ya Rwanda kusitisha uungaji mkono wake kwa kundi la waasi la M23 wakati wa mkutano na waandishi wa habari pamoja na Rais wa DRC Tshisekedi mjini Paris.
Onesphore Sematumba, mchambuzi wa Kundi la Kimataifa la Migogoro, alisema kutekwa kwa Rubaya ni jambo kubwa katika mzozo huo.
"Rubaya ina amana za madini na bila shaka hii itaruhusu M23 kuzinyonya," aliiambia AP.
Kunidi l M23, ni kundi la kijeshi la waasi ambalo liliundwa na kabila la Watutsi, walijitenga na jeshi la DRC zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Walifanya mashambulizi makubwa mwaka 2012 na kuchukua mji mkuu wa mkoa wa Goma karibu na mpaka na Rwanda, mji huo huo ambao wanaotishia tena.