Na Mustafa Abdulkadir
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Baada ya kung'olewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar Hassan Albashir, mnamo 2019, Sudan ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, huku RSF na Jeshi la Sudan wakishindwa kuiongoza nchi hiyo.
Jeshi la Sudan likiongozwa na Abdel Fattah al-Burhan, na Wanamgambo wa RSF waliongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Daglo anayejulikana kama Hemedti. Wawili hao wamekuwa wakioneshana ubabe na kupimana nguvu haswa katika mji mkubwa wa Khartoum, hatua iliyosababisha maelfu ya wananchi kuhamia vijijini na hata nchi jirani, wakihofia usalama wao.
Aidha mapigano hayo yalisambaa hadi mji wa Wad Madani ulioko Kusini Mashariki mwa Khartoum, hali kadhalika Darfur na Kordofan, huku kesi za uporaji wa mali na ubakaji zikiripotiwa.
Je! Juhudi za upatanishi zilifaulu?
Tarehe 11 Mei, Saudi Arabia ilitangaza kufanya mazungumzo ya kusitishwa kwa mapigano na kuruhusu misaada kuingizwa katika miji iliyokumbwa na mapigano haswa Khartoum. Mazungumzo hayo yaliyoongozwa pamoja na Marekani mjini Jeddah, yalileta nafuu na kuruhusu misaada kuingia Sudan japo kwa siku chache, baada ya pande mbili hizo kukiuka makubaliano ya kusitishwa kwa vita.
Mazungumzo yalifanywa tena mnamo 25 Oktoba,2023 mjini Jeddah, wakati huu yakiongozwa pamoja na Muungano wa Maendeleo Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) na wawakilishi wa Umoja wa Afrika. Hata hivyo mazungumzo hayo hayakuwa ya mafanikio, baada ya al-Burhan kujitoa kikaoni kwa madai kuwa mpinzani wake hakuwa na nia ya kutekeleza makubaliano ya hapo awali. Hata hivyo, duru zinasema kuwa pande zote mbili hazikuwa tayari kutekeleza makubaliano yoyote.
Jaribio la tatu la kutafuta suluhu ya mgogoro huo na kuruhusu misaada kuingia Sudan, yalipangwa kufanyika Djibouti, yakiongozwa na muungano wa IGAD. Mchakato huo ulitarajia kuwaleta pamoja al-Burhan na Daglo kwa mara ya kwanza baada ya kuzuka kwa vita. Hata hivyo aliyehudhuria mkutano huo ni al-Burhan pekee, huku Daglo akihudhuria kwa njia ya simu.
Wawili hao walitoa azimio la kukubali pendekezo la kusitishwa kwa vita na kukubali kukutana baada ya siku 15, ingawaje mazungumzo hayo, hadi sasa, yameshindwa kung'oa nanga.
Wanataka nini hasa?
Mpaka sasa mazungumo ya kusitishwa kwa vita hayakuzaa matunda, huku kila kiongozi akivutia kamba upande wake, ambapo kiongozi wa Jeshi la Sudan, al-Burhan akitoa wito wa kuvunjwa kwa vikosi hivyo na kutaka waondoke mara moja kwenye miji wanayoishikilia. Kiongozi huyo, pia ametuhumu RSF kwa kutekeleza mashambulizi tofauti.
Kwa upande wake, kiongozi wa RFS Daglo anataka kuona mageuzi ndani ya Jeshi, akilituhumu jeshi hilo kuendeshwa na wafuasi wa aliyekuwa Rais wa Sudan Omar al-Bashir, na kadhalika ametaka kuundwa kwa serikali ya raia.