Jeshi la Gabon limesema kuwa litafungua tena mipaka ya nchi hiyo ambayo ilifungwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais Ali Bongo.
Msemaji wa watawala wa kijeshi wa Gabon alisema kwenye televisheni ya taifa kwamba "wameamua mara moja kufungua tena mipaka ya nchi kavu, baharini na angani kuanzia Jumamosi hii".
Kundi la wanajeshi 12 wa Gabon walikuwa wametangaza siku ya Jumatano kwamba mipaka ya nchi hiyo imefungwa hadi itakapotangazwa tena, katika taarifa iliyotangazwa na shirika la televisheni ya Gabon 24.
Jenerali Brice Oligui Nguema, mkuu wa walinzi jeshi la kulinda rais, Jumatano aliongoza maafisa katika mapinduzi dhidi ya rais Ali Bongo Ondimba.
Uchaguzi uliozua utata Gabon
Kuondolewa kwa ali Bongo kwa urais, kulikuja muda mfupi tu baada ya yeye kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais mwishoni mwa juma - matokeo yaliyotajwa kuwa si ya haki na upinzani.
Viongozi hao wa mapinduzi walisema wamevunja taasisi za taifa na kufuta matokeo ya uchaguzi pamoja na kufunga mipaka.
Oligui anatarajiwa tarehe 4 Septemba kuapishwa kama "rais wa mpito".
Nchi nyingine tano barani Afrika - Mali, Guinea, Sudan, Burkina Faso na Niger - zimepitia mapinduzi katika miaka mitatu iliyopita.