Viongozi wa nchi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) wamesisitiza kuheshimiwa kwa uhuru na maamuzi ya Somalia kuhusu bandari ya Berbera, mradi ulioghubikwa na utata.
Somaliland, iliyojitenga kutoka Somalia mwaka 1991, iliingia makubaliano ya Ethiopia juu ya matumizi ya bandari hiyo, Januari 1, 2024.
Katika mkutano wao uliofanyika mjini Entebbe nchini Uganda, viongozi hao walitumia muda mwingi kuangazia mzozo wa Somalia na Ethiopia, pia walipata wasaa wa kujadili machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Sudan.
Wakuu hao hawakuficha hofu yao juu ya uhusiano uliozorota kati ya Ethiopia na Somalia."
Viongozi hao waliweka bayana haja ya kuheshimu uhuru, umoja na maamuzi ya Somalia.
Kauli ya Somalia
"... uhusiano wowote unapaswa kuzingatia kanuni kuu zilizo hapo juu, na makubaliano au mpango wowote unapaswa kuwa kwa ridhaa ya Somalia," IGAD ilisema katika taarifa baada ya mkutano wa 42 wa wakuu wa nchi na serikali.
Marais hao walizitaka Ethiopia na Somalia kupunguza mvutano na badala yake washiriki "mazungumzo yenye kujenga na kutafuta suluhu."
Hata hivyo, waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, hakuwemo kwenye mkutano huo, wakati mwenzake wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud alihudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Wengine waliokuwepo kwenye mkutano huo ni pamoja na Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti ambaye pia ni Mwenyekiti wa IGAD, William Ruto kutoka Kenya na Rais wa Sudan ya Kusini, Salva kiir Mayardit.
Mnamo Januari 1, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi waliingia katika makubaliano huko Addis Ababa, yenye kuiruhusu Ethiopia, nchi isiyo na bandari, kufikia bandari ya Berbera.
Kama sehemu ya mpango huo, Somaliland inapanga kukodisha eneo la kilomita 20 kwenye ufukwe wake hadi Ethiopia ili kuanzisha kituo cha jeshi la wanamaji. Somaliland, kwa upande mwingine, iliahidiwa kutambuliwa na Ethiopia.
Ethiopia kwa sasa inategemea nchi jirani ya Djibouti kwa sehemu kubwa ya biashara yake ya baharini. Awali, Ethiopoa ilikuwa na ukanda wa pwani kando ya Bahari Nyekundu, lakini baada ya Eritrea kujitenga mwaka 1993, Ethiopia ilipoteza bandari.
Somalia ilikataa makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Ethiopia na Somaliland, huku ikiyaita ni ya 'kichokozi'.