Waziri Mkuu wa Ethiopia na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy wameongea kwa simu.
"Niliongea kwa simu na rais@ZelenskyyUa leo kujadili masuala ya nchi zetu mbili na kimataifa yenye maslahi pamoja na njia za kuleta amani kati ya Ukraine na Urusi," waziri mkuu amesema katika mtandawo wake wa twitter.
Rais Zelenskyy ametoa mwaliko kwa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuzuru nchi yake.
"Sauti ya Ethiopia, Umoja wa Afrika, Afrika nzima ni muhimu sana kwetu," Zelenskyy alisema, kulingana na taarifa kutoka ofisi yake.
Mwaliko huu umekuja mwezi mmoja baada ya kuwakaribisha marais watatu wa Kiafrika mjini Kiev ambao walikuwa wamependekeza mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi.
Alisisitiza haja ya kuunda jukwaa la mazungumzo na nchi za Afrika.
Simu hiyo ilikuwa ya kwanza kati ya viongozi wa nchi hizo mbili katika historia ya uhusiano wao.
Uhusiano na Afrika
Ukraine na Urusi zimekuwa zikijihusisha na mipango ya kidiplomasia ili kuyashawishi mataifa ya Afrika kuwaunga mkono.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Urusi na Ukraine wote wamezuru barani humo katika muda wa miezi miwili iliyopita.
Zelensky mwezi Juni alikutana na ujumbe wa marais wa Afrika mjini Kiev ambao pendekezo lao lilijumuisha kupunguzwa kwa hali ya juu na hatimaye mazungumzo na Kremlin.
Rais wa Ukraine alifutilia mbali mazungumzo na Urusi huku majeshi yake yakichukua ardhi ya Ukraine.
Mpango wa amani wa Afrika uliongozwa na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Hakainde Hichilema wa Zambia na Azali Assoumani wa Comoro.
Watatu hao pia walikutana tofauti na Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye alisema Ukraine mara zote ilikataa mazungumzo.