Viongozi wa kidini wa Sudan Kusini wameitaka serikali kuendesha uchaguzi kwa wakati.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Episcopal Church of South Sudan (ECSS), Askofu Mkuu Justin Badi Arama, alitoa wito kwa Serikali ya Mpito Iliyohusishwa na Umoja wa Kitaifa na marafiki wa Sudan Kusini kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika bila kuongezwa muda.
Alisema uongozi wa kanisa unaamini hili litahakikisha kuwa maisha ya wananchi wasio na hatia hayawekwi hatarini.
“Sote tunakubaliana kwamba uchaguzi lazima ufanyike. Hata hivyo, tuna wasiwasi mkubwa kwamba mahitaji mengi muhimu ya mchakato wa uchaguzi hayatekelezwi kikamilifu,'' Arama alisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano.
Rais Salva kiir kugombania kiti
Alisema alitoa mfano wa mipangilio inayohitajika kama ya usalama, kuundwa upya kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kufadhiliwa kwa bajeti ya uchaguzi, kuwarejesha makwao wakimbizi na kuwarejesha nyumbani waliorejea, na kuundwa upya kwa baraza la vyama vya siasa.
''Tunasema kwamba kabla ya uchaguzi, sharti zote hizi zitekelezwe kikamilifu," alisema.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir mapema mwezi huu aliahidi kufanya uchaguzi wa kwanza nchini humo tangu uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2002.
Rais Kiir alisema atawania wadhifa wa juu zaidi wa taifa kama mpeperushaji bendera wa chama chake cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM).
Kiir alisisitiza kuwa hakutakuwa na nyongeza zaidi ya kipindi cha mpito pindi kitakapokamilika mwaka wa 2024.
Sudan Kusini imepanga kufanya uchaguzi mkuu mwezi Desemba 2024.