Viongozi wa Afrika wasema kuwe na mtindo mpya wa kifedha kufadhili mifumo ya chakula

Viongozi wa Afrika wasema kuwe na mtindo mpya wa kifedha kufadhili mifumo ya chakula

Marais wa Afrika wamehudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mfumo wa Chakula
Viongozi kutoka Afrika wamehudhuria mkutano wa UN wa Mfumo wa Chakua nchini Italy / Photo from Villa Somalia

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud anasema Afrika inahitaji mbinu mpya ya kufadhili mifumo ya chakula.

Rais ameongea katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mfumo wa chakula unaofanyika Italy (UN Food Systems Summit +2),

"Leo dunia inakabiliwa na changamoto na hali tofauti kuliko ilivyokuwa miongo kadhaa iliyopita," Rais Mohamud amesema, " tunachohitaji ni mtindo mpya na wa kiubunifu wa kufikia taasisi za fedha za kimataifa katika nchi nyingi za Afrika na hasa katika nchi dhaifu kama Somalia."

Somalia ni kati ya nchi ambazo zinakumbwa na ukame wa miaka mingi .

Shirika la chakula duniani lasema zaidi ya watu milioni sita na laki tano wameathiriwa na ukame, ambao umeletwa na athari ya tabianchi.

"Tunahitaji mbinu mpya ya kugharamia mifumo ya chakula si ule mfumo wa kawaida, iliyokuwepo na benki ya dunia, kwa ya maendeleo ya Afrika na kila aina ya taasisi za kifedha ambazo tumekuwa tukitumia," rais aliongezea.

Rais Mohamud amesema Somalia ina uwezo wa kujilisha kwa kutumia kilimo cha ardhi , uvuvi, mifugo na rasilimali nyingine lakini changamoto ya ukosefu wa usalama umeifanya kukosa kujimudu ipasavyo.

Kenya imeongeza sauti kwa wito huu ikiwa pia ina changamoto ya ukame kama Somalia.

Takiwmu zaonyesha zaidi ya watu milioni nne na laki nne wamelazimika kutegemea usaidizi wa chakula.

"Tunatoa wito kwa wafadhili waangalie bara la Afrika kwa njia tofauti," Gachagua ameongezea, " wanafaa kuwekeza fedha kando kwa ajili ya Afrika ili kuiwezesha bara kuzalisha chakula cha kutosha na kuwa na ya ziada ya kuuza."

Mkutano wa viongozi na wataalamu nchini Italy unafanyika kutoka 24 had 26 Julai.

Ina nia ya kutambua maeneo muhimu ya kipaumbele kwa lengo la kimataifa katika miaka miwili ijayo.

Hii ni pamoja na jinsi ya kuhamasisha ufadhili, kujenga ujuzi na uwezo miongoni mwa wataalam wa mifumo ya chakula na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kikanda na kitaifa kwa ajili ya hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

TRT Afrika