Viongozi wa Afrika wanakutana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kwa mazungumzo juu ya kuongeza utekelezaji wa makubaliano ya eneo la biashara huru kote barani.
Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) linalenga kuongeza biashara kati ya majirani wa Kiafrika na lengo lake ni kuunganisha watu bilioni 1.3 katika eneo lenye thamani ya dola trilioni 3.4 kiuchumi.
Lengo lake ni kuwa eneo kubwa zaidi la biashara huria duniani, likiunganisha nchi 54.
"Soko hili moja litawatoa watu milioni 30 kutoka katika umaskini mkubwa na kuongeza kipato," alisema Rais wa Kenya, William Ruto.
Mkutano huo unahudhuriwa na Abdel Fatah El-Sisi wa Misri, Bola Tinubu wa Nigeria, Ali Bongo Ondiba wa Gabon, Macky Sall wa Senegal, na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wengine ni Rais Azali Assoumani wa Comoros na Ismail Omar Guelleh wa Djibouti.
Majadiliano yatakuwa kati ya Umoja wa Afrika na vikundi vya kikanda kuhusu utekelezaji wa muungano wa bara hilo. Vikundi hivyo vitaelezea hatua zilizochukuliwa mwaka huu.
Vikundi vya kikanda ni Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mamlaka ya Serikali za Kikanda (IGAD), na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).
Nchi za Kiafrika zilianza biashara rasmi chini ya AfCFTA tarehe 1 Januari 2021.
Biashara kati ya mataifa ya Kiafrika inachangia takriban 10% ya biashara yote ya bara hilo lenye mataifa 55, ambayo imepungua kidogo katika kipindi cha muongo uliopita na ikilinganishwa na 25% katika Asia ya Kusini-Mashariki.
Rais wa Kenya, William Ruto, aliitaka Jumuiya ya Afrika kufanyiwa mageuzi ili iwe huru zaidi.
"Tunapaswa kuifungua AU kutoka kwenye vikwazo ili iweze kutekeleza hatua muhimu na za dharura katika bara hili kwa kutumia rasilimali zinazozalishwa ndani," alisema Ruto.
"Utegemezi wa muda mrefu kwa washirika wenye nia njema hauendani na ndoto hii."