Watoto walioko katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam wako hatarini kufuatia vita vinavyoendelea Sudan. /Picha: Reuters

Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vilianzisha upya mashambulizi yake kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam ilioko katika jimbo la Darfur Kaskazini siku ya Jumatano.

Gavana wa Darfur Kaskazini, Minni Arko Minawi amesema kuwa RSF "imeshambulia kambi ya Zamzam kwa mara ya pili ndani ya siku mbili."

Kwa mujibu wa taarifa, RSF ilianzisha mashambulizi makali kwenye kambi hiyo siku ya Jumanne, na kufanya unyanyasaji mkubwa dhidi ya raia, kuteketeza soko kuu na kupora magari na mali za waliokimbia makazi yao.

Hata hivyo Jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limepambana na shambulio hilo.

Minawi ametoa wito kwa jumuiya za kimataifa na kikanda "kuzingatia matukio haya mabaya na mauaji ya halaiki yanayofanywa na wanamgambo (RSF) dhidi ya wakazi wa kambi hiyo."

Vile vile Gavana huyo, ambaye anasimamia kikosi cha pamoja, alituma ujumbe kupitia ukurasa wake wa Facebook: "Tunatoa wito kwa wale wote wanaoweza kuwa na silaha kuwaokoa watu wetu waliokimbia makazi yao kutokana na ukatili wa wanamgambo wa kigaidi wa RSF na kulinda ardhi na heshima."

Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema maelfu ya watoto walioko katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam, huko El Fasher, magharibi mwa Sudan wako hatarini.

Katika taarifa fupi kupitia mtandao wa X, UNICEF Sudan ilisema: "Mamia ya maelfu ya watoto wako hatarini huku mapigano yakiongezeka ndani na karibu na El Fasher na kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini nchini #Sudan."

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) pia limeonesha wasiwasi wake kuhusu mashambulio hayo, limesema : "Wakati RSF inazidisha mashambulizi karibu na El Fasher na kambi ya Zamzam, MSF ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa wafanyakazi wake na maelfu ya watu ambao tayari wanashambuliwa na wana tatizo la njaa katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi ya Sudan."

Majeshi ya Sudan na RSF yamekuwa yakipigana tangu Aprili 2023, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000, huku karibu watu milioni 15 wakikimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa na serikali za mitaa.

TRT Afrika na mashirika ya habari