Vincent Meriton alikuwa Makamu wa Rais wakati wa uongozi wa Danny Faure kutoka 2016 hadi 2020. Picha wengine 

Serikali ya Ushelisheli imetangaza rasmi kuweka mgombea atakaewania nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika. Makamu wa Rais Vincent Meriton ndie aliyeteuliwa katika kinyang'anyiro hicho.

Hatua hii inaongeza idadi ya wagombea ambao tayari washajitokeza na kufikia nchi nne. Mbali na Ushelisheli, nchi nyengine ni Kenya, Somalia na Djibouti. Ushelisheli imemmwagia sifa mgombea wake na kusema ni mtu mwenye ukomavu wa kisiasa.

Itakumbukwa kwamba, Meriton amewahi kushikilia nyadhifa nyingi serikalini, ikiwemo nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje, Afya na Masuala ya Jamii, Teknolojia ya Habari, Uchumi wa Bluu na Maendeleo ya Ujasiriamali.

Meriton pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wakati wa uongozi wa Danny Faure kutoka 2016 hadi 2020.

Serikali yake imeongeza kusema kuwa Meriton pia amewahi kuiwakilisha Ushelisheli katika kutetea nafasi kwenye Uchumi wa Bluu katika nyanja za kimataifa.

Anaangaliwa kama mwanasiasa mwenye uwezo wa kuboresha kwa kiasi kikubwa kiwango cha utekelezaji wa maamuzi ya utendaji wa Tume ya AU kwa kushughulikia vikwazo vya utekelezaji na kukuza uwajibikaji.

Mwenyekiti wa Tume huchaguliwa na viongozi wa Afrika kwa muda wa miaka minne na iwapo atachaguliwa tena anaweza kuhuduma kwa awamu ya pili.

Iwapo atachaguliwa, Meriton atamrithi Moussa Faki Mahamat kutoka Chad. Vincent Meriton sasa anakiangalia kiti hicho cha juu cha Umoja wa Afrika, huku Kenya pia ikikitaka kupitia waziri mkuu wake wa zamani Raila Odinga, wakati huo huo Somalia nayo imemteuwa Fawzia Yusuf Adam mwanadiplomasia wa nchi hiyo.

Na Djibouti nayo imemuweka Mahamoud Ali Youssouf ambae ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo. Ni wakati wa Afrika Mashariki kuteuliwa katika nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika katika uchaguzi utakaofanyika Februari 2025.

Swali ni, Ushelisheli itakuwa ndio ya mwisho kuweka mgombea, au bado kuna nchi nyengine zitakazojitokeza? Mtego uliopo ni iwapo, nchi za Afrika Mashariki hatimae zitaweza kuweka mgombea mmoja atakae peperusha bendera ya kanda ya Afrika Mashariki.

TRT Afrika