Wasafiri kutoka Kenya, Eswatini na Zimbabwe sasa wanaweza kuingia nchini Urusi wakiwa na viza za kielektroniki, kulingana na tangazo la hivi majuzi la Ubalozi wa Urusi nchini Kenya.
"Serikali ya Urusi imeongeza orodha ya nchi ambazo raia wake wanaweza kutembelea Shirikisho la Urusi na viza moja ya kielektroniki. Orodha hiyo sasa inajumuisha nchi zifuatazo za Kiafrika: Kenya, Eswatini na Zimbabwe," ubalozi ulisema Jumapili katika taarifa juu ya X.
"Maendeleo hayo yanatarajiwa kuwezesha usafiri kati ya Urusi na nchi hizo, kukuza utalii, biashara na kubadilishana utamaduni," imesema Mamlaka.
Kulingana na Urusi, e-Visa inawapa raia wa nchi hizo tatu haki ya kuingia Urusi mara moja na kuwaruhusu kukaa hadi siku 16.
Uhusiano wa Urusi na Afrika
Viza ni halali kwa siku 60 kutoka tarehe ya usajili na inaweza kutumika kwa madhumuni mbalimbali.
Kuanzishwa kwa sera ya eVisa ni hatua muhimu kuelekea kurahisisha taratibu za usafiri na kukuza diplomasia ya mtu-kwa-mtu kati ya Urusi na Afrika.
Urusi imezidi kuboresha uhusiano na mataifa mengi ya Afrika. Mwezi Julai, Urusi iliandaa Mkutano wa Urusi -Afrika na Jukwaa la Kiuchumi na Kibinadamu la Urusi-Afrika, ambalo uliwaleta pamoja wakuu wa nchi na serikali, wajasiriamali, wasomi na watu mashuhuri wa umma.
Siku ya Jumatatu, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitangaza kuundwa kwa mfuko maalum wa maendeleo ya ushirikiano kati ya Urusi na Afrika.