Kiongozi wa Muungano wa Azimio One Kenya na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga anasisitiza kuwa pendekezo la Rais William Ruto la kutumia utaratibu wa bunge kushughulikia matatizo yaliyoletwa na upinzani wakati wa maandamano ya hivi karibuni huenda lisifanikishe uuwiano mwema.
Uongozi wa Azimio unataka kuanzisha mazungumzo ya kitaifa kwa kutumia utaratibu sawa na Mkataba wa Kitaifa wa 2008, ambao ulipatanishwa na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa marehemu Koffi Annan kutokana na machafuko yaliyotokana na uchaguzi wa rais wa 2007.
Katika pendekezo lake la mageuzi ya uchaguzi na suluhu la gharama ya juu ya maisha nchini, Raila aliomba watu kutoka nje ya bunge waruhusiwe kushiriki mazungumzo hayo.
Odinga pia katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliomba kwamba serikali ilipe ada za matibabu kwa yeyote aliyeumizwa wakati akishiriki maandamano ya upinzani.
"Tumeazimia kwamba serikali lazima ichukue gharama mara moja au iondoe bili zote za matibabu ya waathiriwa wa ukatili wa polisi wakiwemo wanahabari, na gharama ya wale waliopoteza maisha," Raila alisema.
Viongozi wa chama tawala cha United Democratic Alliance wamekerwa na matakwa haya mapya. Baadhi wanadai kuwa Raila Odinga aliwasilisha matakwa mapya katika juhudi za kuhujumu makubaliano ya amani aliyoafikiana na Rais William Ruto awali.
Raila ameshikilia kuwa iwapo matakwa yake hayatatekelezwa, hatasita kuitisha maandamano zaidi tena.
"Tutarejea kwa wananchi iwapo matakwa yetu hatatiliwa maanani ," alisema.