Shirika hilo la kitamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO limeonyesha hofu kuhusu ripoti za makundi yenye silaha kupora maeneo ya makumbusho na taasisi za urithi Sudan wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vikiendelea.
Sudan imekumbwa na vita kati ya Jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces , RSF, tangu Aprili 2023.
"UNESCO ina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za hivi karibuni za uwezekano wa uporaji na uharibifu wa makumbusho kadhaa na taasisi za urithi nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na Makumbusho ya Kitaifa, na makundi yenye silaha," UNESCO ilisema.
Shirika hilo limesema limekuwa likifuatilia athari za vita katika maeneo ya urithi wa Sudan, taasisi za kitamaduni na wasanii tangu uhasama ulipozuka mwaka 2023.
"Katika wiki za hivi karibuni, tishio hili kwa tamaduni linaonekana kufikia kiwango ambacho hakijawahi kutokea, na ripoti za uporaji wa makumbusho, urithi na maeneo ya ikolojia na makusanyo kibinafsi ya vito vya utamaduni."
Imetoa mfano wa ripoti za uporaji katika Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Sudan, pamoja na Makumbusho ya Khalifa House huko Omdurman na Makumbusho ya Nyala huko Darfur Kusini.
Jumba la Makumbusho la Kitaifa, ambalo lilifunguliwa katika miaka ya 1970, limekuwa eneo la hifadhi kwa zaidi ya kumbukumbu 2,700 vikiwemo vipande muhimu kutoka nasaba za kale za Mafarao wa Misri na utamaduni wa Wanubi.
"UNESCO inasisitiza wito wake kwa umma na soko la sanaa linalohusika na biashara ya mali ya kitamaduni katika kanda na duniani kote kuacha kununua au kushiriki katika kuagiza, kuuza nje au kuhamisha umiliki wa mali ya kitamaduni kutoka Sudan," ilisema.