Vita nchini Sudan vimelazimisha zaidi ya watu milioni saba kutoroka makwao.  Picha: AFP

Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, Martin Griffiths, anasema kuwa mwaka huu wa 2024, jumuiya ya kimataifa - hasa zile zenye ushawishi kwa wahusika katika mzozo nchini Sudan zinafaa kuchukua hatua ya kukomesha vita nchini Sudan.

Vita nchini humo vilianza 15 Aprili 2023 kati ya jeshi la serikali inayoongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kikundi cha Rapid Support Forces kinachoongozwa na jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

Griffiths katika taarifa anasema kuna umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti na za haraka kukomesha mapigano na kulinda operesheni za kibinadamu zinazokusudiwa kusaidia mamilioni ya raia.

"Kote Sudan, takriban watu milioni 25 watahitaji usaidizi wa kibinadamu mwaka 2024. Lakini ukweli ni kwamba kuongezeka kwa uhasama kunawaweka wengi wao nje ya uwezo wetu. Uwasilishaji wa huduma katika maeneo ya migogoro umesitishwa," Griffiths amesema.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 7.3 wamekimbia makazi yao ndani na nje ya Sudan tangu mapigano yazuke15 Aprili 2023.

Idadi ya watu waliokimbia makazi yao ndani ya Sudan imeongezeka kwa takriban 500,000 katika muda wa mwezi mmoja, hasa kutokana na migogoro katika sehemu za Aj Jazirah na majimbo mengine.

"Kwa kuwa sasa uhasama umefikia eneo la uzalishaji chakula cha nchi katika Jimbo la Aj Jazirah, kuna hatari zaidi. Zaidi ya watu 500,000 wamekimbia mapigano ndani na karibu na mji mkuu wa jimbo la Wad Medani, ambalo ni kimbilio la muda mrefu kwa wale waliozuiliwa na mapigano mahali pengine," Griffiths ameongezea.

Ukosefu wa usalama, uporaji, vikwazo vya urasimu, mtandao duni na mawasiliano ya ya simu, ukosefu wa fedha taslimu, na wafanyakazi wachache wa kiufundi na wa kibinadamu vinaathiri utoaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo mengi ya nchi.

"Kwa watu wa Sudan, 2023 ulikuwa ni mwaka wa mateso. Mnamo 2024, wahusika katika mzozo lazima wafanye mambo matatu kuumaliza: Kulinda raia, kuwezesha ufikiaji wa huduma za kibinadamu, na kukomesha mapigano - mara moja," Griffiths amesema.

Wanaotoa misaada nchini humo pia wanahofia kuwa uhamisho wa watu wengi unaoendelea pia unaweza kuchochea kuenea kwa haraka kwa mlipuko wa kipindupindu katika jimbo hilo, huku zaidi ya kesi 1,800 zinazoshukiwa zimeripotiwa huko hadi sasa.

Disemba 2023 majenerali wanaozozana walionyesha hamu ya kufanya mazungumzo ya amani lakini bado mikakati na wakati wa kuanza kwa maongeza haya haujathibitishwa.

.

TRT Afrika