Baadhi waathirika wa mauaji ya kimbari katika kumbukumbu ya picha./Picha: AP

Mwendesha Mashtaka mkuu wa Mfumo wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (MICT), Serge Brammertz amewasili nchini Rwanda, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kutafuta haki kwa waathirika wa mauaji ya kimbari yaliyotokea miaka 30 iliyopita.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na MICT, Brammertz atakuwa nchini Rwanda kuanzia Januari 30 mpaka February 7, 2024.

"Brammertz atakuwa nchini Rwanda kwa mkakati maalumu wa kutafuta haki kwa waathirika wa mauaji hayo, akiendesha mijadala na jitihada mbalimbali za kutafuta haki kwa waathirika hao," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mwendesha Mashtaka wa mahakama ya IRMCT Serge Brammertz yupo Rwnda kwa ziara rasmi / Picha kutoka IRMCT

Zaidi ya Wanyarwanda milioni moja waliuawa kikatili ndani ya siku 100 wakati wa Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi ya 1994.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya washukiwa 1,000 wako mafichoni katika sehemu mbalimbali duniani, ikiwemo Afrika, Ulaya na Amerka.

Umoja wa Mataifa una amini kuwa uwepo wa watuhumiwa wengi kiasi hicho mafichoni, unawaongezea machungu waathrika hao na kufifisha dhana ya utawala wa sheria nchini humo.

Akiwa Rwanda, Mwendesha Mashtaka huyo atakutana na mamlaka za kisheria za nchi hiyo kutafuta namna ya kuwasaidia waathirika wa mauaji hayo kwa kuwafichua washukiwa hao, popote pale walipo.

"Brammertz yuko tayari kukutana na Waziri wa Sheria, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mwendesha Mashtaka wa nchi hiyo kutafuta muafaka wa kuwafikia watuhumiwa na kuwaleta kwenye mkono wa sheria," ameongeza.

TRT Afrika