Sudan iko ukingoni mwa "vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe" ambavyo vinaweza kuathiri eneo lote, Umoja wa Mataifa ulionya Jumapili, baada ya shambulio la anga kwenye eneo la makazi na watu zaidi ya ishirini kuripotiwa kuuawa.
Wizara ya afya ya Sudan iliripoti "waliofariki ni 22 na kuna idadi kubwa ya waliojeruhiwa miongoni mwa raia" kutokana na mgomo katika mji wa Omdurman, katika wilaya ya Dar al-Salam, ambayo ina maana "Nyumba ya Amani" kwa Kiarabu.
Takriban watu 3,000 wameuawa katika vita hivyo kote Sudan vilivyoanza Aprili, Kumekuwa na uporaji mkubwa na ripoti za unyanyasaji wa kijinsia huku Umoja wa Mataifa ukionya kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa haki za kibinadamu katika eneo la Darfur.
Video iliyotumwa na wizara ya afya kwenye mtandao wa Facebook ilionyesha miili ya waliokufa baada ya shambulio hilo la anga, wakiwemo wanawake kadhaa. Msimulizi anasema kuwa wakazi "walihesabu watu 22 waliofariki".
Sheria hazijaheshimiwa
Baada ya takriban miezi mitatu ya vita kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Rapid Support Forces, shambulio hilo la anga ni tukio la hivi punde zaidi kuibua hasira za kimataifa, kulingana na ripoti za shirika la habari la AFP.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Jumapili alilaani shambulizi la anga la Omdurman.
Shambulio hilo la anga "limeripotiwa kuua takriban watu 22" na kujeruhi makumi, naibu msemaji wake Farhan Haq alisema katika taarifa.
Guterres "ana wasiwasi mkubwa kwamba vita vinavyoendelea kati ya vikosi vya kijeshi vimeipeleka Sudan kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vinaweza kuathiri kanda nzima," Haq alisema.
Tangu vita kati ya jeshi na vikosi vya Rapid Support Forces kuanza mwezi wa Aprili, kumekuwa na ''kupuuzwa kabisa kwa sheria za kibinadamu na haki za binadamu jambo ambalo ni hatari na linasumbua," aliongeza.
Juhudi zilizofanywa upya
Kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, takriban watu milioni tatu wameathiriwa na mapigano ya Sudan, miongoni mwao wakiwa takriban 700,000 ambao wamekimbilia nchi jirani,
Haq alielezea kuunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki IGAD kumaliza mgogoro wa Sudan.
Viongozi wa Ethiopia, Kenya, Somalia na Sudan Kusini - wanachama wa IGAD wanaoshughulikia suala la Sudan - watakutana mjini Addis Ababa siku ya Jumatatu.
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo wamealikwa lakini hakuna upande uliothibitisha kuhudhuria.
Mikakati mingi ya kusitisha mapigano katika vita hivyo imetangazwa lakini imepuuzwa kwa kiasi kikubwa.