Takriban watu 12,000 wamepoteza maisha kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan./ Picha: AP

Umoja wa Mataifa umeanza uchunguzi kuhusu tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu kufuatia machafuko ya kisiasa ambayo yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 12,000 na kuwaacha mamilioni wengine bila makazi.

"Mashirika ya kiraia ya Sudan na watu wengine wameanza kutoa taarifa kuhusu madai ya ukiukwaji mkubwa unaoendelea," alisema Mohamed Chande Othman, mwenyekiti wa Ujumbe wa kutafuta ukweli nchini humo.

“Mashirika ya kiraia ya Sudan na wadau wengine wameanza kushiriki nasi madai ya ukiukaji mkubwa wa haki unaoendelea. Madai haya yanasisitiza umuhimu wa uwajibikaji, umuhimu wa uchunguzi wetu, na umuhimu wa kumaliza ghasia hizi kwa wakati.”

Mbali na Othman, ambaye ni Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania, ujumbe huo pia unaongozwa na Joy Ezeilo, mtaalamu wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nigeria na Mona Rishmawi, na mtaalamu wa mambo wa Sheria wa Umoja wa Mataifa kutoka Jordan.

'Majukumu ya kisheria'

"Pande zinazopigana zina wajibu wa kisheria wa kimataifa kulinda raia dhidi ya mashambulizi, kuhakikisha upatikanaji wa kibinadamu na mauaji yanasababisha watu kukimbia makazi yao ," alisema Rishmawi.

"Madai yote yatafanyiwa kazi na tutafanya uchunguzi wetu kwa uhuru wote bila hofu wala upendeleo."

Uchunguzi huo utaangazia madai yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusisha mzozo katia ya Jeshi la Sudan (SAF), Vikosi vya RSF, na pande zingine zinazopigana tangu kuanza kwa vita hivyo, Aprili 15, 2023.

Kwa upande wake, Joy Ezeilo alisema ujumbe huo kutoka Umoja wa Mataifa utazingatia zaidi ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa kwa wanawake na watoto.

Mwaliko wa kushiriki kutoa ushahidi

"Madai ya ubakaji yanayolenga hasa wanawake na wasichana na madai ya kuajiri watoto kwa ajili ya matumizi ya vita ni miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele katika uchunguzi wetu," alisema Ezeilo.

Umoja wa Mataifa umeziasa pande zinazohasimiana kutoa ushurikiano wa kutosha kwa ujumbe huo na kuwataka watu binafsi, makundi na mashirika mengine kuwasilisha kwa siri, shuhuda za ukiukwaji wa haki hizo.

Ujumbe huo utawasilisha taarifa ya matokeo ya awali katika kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu mwezi Juni-Julai 2024, ikifuatiwa na ripoti ya kina kwa kikao cha 57 cha Baraza hilo mwezi Septemba-Oktoba na kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha 79 mwezi Oktoba 2024.

Zaidi ya watu 13,000 wameuawa tangu vita vilipoanza mwezi wa Aprili, kulingana na makadirio ya shirika la Armed Conflict Location and Event Data Project, wakati Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni saba wameyakimbia makazi yao.

TRT Afrika