Maafisa wakuu wa UN wamelaani ripoti zinazoongezeka za unyanyasaji wa kijinsia nchini Sudan.
Vita nchini humo vinaendelea tangu Apriili kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya Rapid Support Forces, RSF.
Umoja wa Mataifa unasema hata kabla ya vita kuanza zaidi ya wanawake na wasichana milioni tatu nchini Sudan walikuwa katika hatari ya unyanyasaji wa kijinsia.
Makadirio ya idadi hii sasa imepanda hadi watu milioni 4.2 tangu vita ianze.
"Timu zetu katika eneo hili zinaelezea visa vya kutisha wanayokabilia ambazo wanawake na wasichana waliohamishwa wanakabiliwa nayo kwa nguvu wakati wakitoroka Sudan," Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi amesema, " Hali hii ya kushangaza ya ukiukaji wa haki za binadamu lazima iishe."
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan imepokea ripoti za kuaminika za matukio 21 ya unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro dhidi ya angalau wanawake na wasichana 57.
Kati ya walioathiriwa ni wasichana wadogo wasiopungua 10. Katika kisa kimoja, wanawake wapatao 20 waliripotiwa kubakwa katika shambulio hilo hilo.
"Hali nchini Sudan hasa katika eneo la Darfur, ni mbaya na ukatili mkubwa unaofanywa dhidi ya raia. Wanawake na wasichana lazima walindwe dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia. Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia masuala haya," mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani.
Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la watoto, UNICEF anasema kuna ongezeko ya ukatili wa kijinsia .
"Lakini mara nyingi sana ukiukaji wa haki za binadamu unaofichwa, unaweza kuwa na madhara makubwa ya kimwili na kiakili ya muda mrefu kwa waathirika. Ni muhimu kubuni mipango ya kuzuia na kukabiliana nayo kwa wanawake na wasichana waathirika, " amesema.
Mashirika ya Umoja wa mataifa yanasema mpango wa kukabiliana na mahitaji ya Kibinadamu Sudan sasa unahitaji dola milioni 63.
Hii itasaidia kufadhili huduma za kuzuia na kukabiliana na waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia nchini Sudan, unaolenga kuwafikia watu milioni 1.3.