Mwenyekiti ya Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat anatoa wito wa utulivu na kuheshimiana ili kupunguza mvutano unaoendelea kati ya Serikali za Ethiopia na Somalia.
Somalia imekataa makubaliano baina ya Ethiopia na eneo lake lililojitenga la Somaliland kuiruhusu kutumia bandari kubwa yenye ufikiaji wa Bahari Nyekundu, ikisema makubaliano hayo hayana nguvu za kisheria.
Iwapo makubaliano hayo yatafanya kazi, yatairuhusu Ethiopia, kukodisha kilomita 20 kuzunguka bandari ya Berbera, ambayo iko kwenye Ghuba ya Aden na ufikiaji wa Bahari Nyekundu, kwa miaka 50 kwa jeshi lake la majini na malengo ya kibiashara.
Somalia, ambayo inaiona Somaliland kama sehemu ya ardhi yake, pia ilimuita balozi wake nchini Ethiopia kwa ajili ya kujadiliana kuhusu makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi siku ya Jumatatu.
Umoja wa Afrika unaitambua Somalia na sio Somaliland kama mwanachama wake.
Mwenyekiti wa Tume ya AU, Faki anasema amekuwa akifuatilia kwa karibu mvutano uliotokana na kusainiwa kwa mkataba kati ya Ethiopia na Somaliland.
Katika taarifa yake, "Anazitaka nchi hizo mbili kujiepusha na kitendo chochote ambacho bila kukusudia kinaweza kusababisha kuzorota kwa uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili jirani za Afrika Mashariki."
Kwa upande wake, kiongozi wa Somaliland alisema Ethiopia inaitambua Somaliland kama taifa huru, na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo.
Hata hivyo, Somalia ilitaja makubaliano hayo kama "uchokozi" na kuapa kutetea eneo lake.
Faki ameongezea kuwa "Anasisitiza umuhimu wa kuheshimu umoja, uadilifu wa eneo na mamlaka kamili ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika mkiwemo Ethiopia na Somalia."
Ameomba nchi hizo mbili kuzingatia kanuni za ujirani mwema ili kukuza na kuimarisha amani, usalama na utulivu katika eneo la Pembe ya Afrika.
Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller amesema, "Marekani inatambua uhuru na uadilifu wa eneo la Somalia ndani ya mipaka yake ya 1960."