Umoja wa Afrika umempongeza mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye kwa ushindi wake katika uchaguzi wa urais ambao matokeo yake yamepata uungwaji mkono mkubwa.
Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema "anampongeza" Faye kwa kutangazwa rasmi mshindi kwenye duru ya kwanza na kumtakia "mafanikio katika uongozi wake."
Kwa mujibu wa matokeo ya awali, Faye alishinda katika duru ya kwanza ya kura kwa asilimia 54.3, na kumtupa mbali kabisa mgombea aliyeungwa mkono na rais aliye madarakani Macky Sall ambae ni waziri mkuu wa zamani Amadou Ba.
Mahakama ya Katiba ya Senegal inaweza kumtangaza Faye kama mshindi rasmi kabla ya mwisho wa juma, ambayo itarahisisha makabidhiano ya madaraka kabla ya Aprili 2, muda rasmi wa kumalizika kwa utawala wa Sall.
Faye, 44, aliachiwa huru kutoka gerezani siku 10 tu kabla ya uchaguzi, pamoja na mwalimu wake katika siasa Ousmane Sonko, ambae alizuiwa kushiriki katika uchaguzi kufuatia mashtaka ya uhalifu ambayo anasema yalichochewa na sababu za kisiasa.