Rais Macky Sall anayemaliza awamu yake ya pili ya urais / Picha: Reuters

Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika , Moussa Faki Mahamat amempongeza rais wa Senegal Macky Sall kwa uamuzi wake wa kutogombea tena urais wa nchi hiyo.

"Napongeza uamuzi wa busara wa kaka yangu, rais Macky Sall wa kutogombea uchaguzi wa urais wa 2024," Faki alisema kupitia mtandao wa twitter.

"Mwanasiasa huyo ameweka mbele maslahi ya Senegal na hivyo kuhifadhi mtindo wa kidemokrasia wa Senegal ," Faki emeelezea.

Rais Macky Sall anayemaliza hatamu yake ya pili ya urais alielezea uamuzi wake katika hotuba kwa wananchi Jumatatu.

Uvumi kwamba Rais wa Senegal alikuwa akipanga kurefusha utawala wake umechochea mvutano wa kisiasa nchini humo.

"Wananchi wenzangu wapendwa, uamuzi wangu baada ya kufikiria kwa muda mrefu ni kutokuwa mgombea katika uchaguzi wa Februari 25, 2024. Senegal ni kubwa zaidi yangu, na imejaa viongozi wenye uwezo kwa maendeleo ya nchi," rais wa Senegal Macky Sall alisema.

Matamshi ya Sall yalikuja kutokana na hofu kwamba alikuwa akipanga kuwania muhula wa tatu kinyume ya katiba.

Wafuasi wa kiongozi mkuu wa upinzani Ousmane Sonko ambaye hivi majuzi alipatikana na hatia ya kupotosha vijana, wamekuwa wakiongeza shinikizo kwa rais kutowania muhula mwingine wa uongozi wakisema kufanya hivyo kutakuwa kinyume na katiba.

Rais Sall aliwataka raia wa Senegal kudumisha amani kabla ya uchaguzi, akisema: "Hebu tuachane na misimamo ya watu wengi ambayo wanataka kuwasilisha nchi yetu kama jangwa lisilo na sheria. Tunaweza kukosa kuelewana kwa mambo kadhaa , lakini sisi sio maadui.”

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres pia alitoa ''shukurani zake kwa Rais Macky Sall na umahiri alioyoonyesha.''

Viongozi wa Afrika Magharibi pia wamempongeza Rais Sall.

Rais wa Niger Mohammed Bazoum alisema ''Ninaelezea matumaini kwamba uamuzi huu uliofikiriwa kwa makini utatuliza hali ya kisiasa katika nchi hii ya ndugu zetu.''

Nchi kadhaa za Afrika Magharibi zimeshuhudia mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni. Na hii imechangiwa na baadhi ya viongozi kukosa kuheshimu katiba juu ya suala la mihula ya rais.

TRT Afrika