Wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Somalia wameratibiwa kuondoka Somalia kufikia Desemba 2024 / Picha: AFP

Umoja wa Afrika umeutaka Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo vya silaha vilivyowekewa Somalia miaka 31 iliyopita.

Umoja wa Afrika inasema hii itawezesha jeshi la Somalia kutoa ulinzi wa kutosha kwa raia baada ya ujumbe wa kulinda amani wa umoja huo kuondoka Somalia.

Wanajeshi wa Umoja wa Afrika katika taifa hilo la pembe ya Afrika wameratibiwa kuondoka Somalia kufikia Desemba 2024, wanajeshi tayari wamenza kuondoka.

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa liliiwekea Somalia vikwazo vya silaha mwaka 1992 kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na ghasia za kiukoo.

Kizuizi hicho kiliondolewa kwa kiasi mwaka wa 2013 ili kusaidia vikosi vya usalama vya Somalia kupambana na ugaidi.

''Ombi la kuondolewa kwa vikwazo vya silaha kutaisaidia Somalia katika mapambano yake ya muda mrefu dhidi ya waasi wa Al-Shabaab,'' Mohamed Al-Amine Souef, mkuu wa ujumbe wa AU nchini Somalia, alisema Alhamisi, wakati wa mkutano na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.

TRT Afrika