Uingereza inakusudia kuanza kuwasafirisha waomba hifadhi nchini Rwanda Julai 24, wakili wa serikali amesema.
Hata hivyo, mpango huo unaopingwa vikali unategemea Chama cha Conservative cha Waziri Mkuu Rishi Sunak kushinda katika uchaguzi ujao.
Kutuma waomba hifadhi ambao wamefika Uingereza bila kibali nchini Rwanda ni mojawapo ya sera kuu za Sunak, lakini vikwazo vya kisheria na bunge vimeisimamisha.
Sunak amesema safari za ndege za uhamisho hazitaondoka kabla ya uchaguzi wa Julai 4 lakini ameahidi ikiwa atashinda zitaanza haraka iwezekanavyo.
Chama cha upinzani cha Labour, kinachoongoza kwa takriban alama 20 katika kura za maoni, kimeahidi kuutupilia mbali mpango huo iwapo kitachaguliwa.
Katika hati zilizowasilishwa kwa Mahakama Kuu ya London kama sehemu ya kupinga sera hiyo na Shirika la Misaada la Asylum Aid, mawakili wa serikali walisema nia ilikuwa "kuondoka kwa ndege hadi Rwanda tarehe 23 Julai 2024 (na sio kabla).
Walakini, wakili wa serikali Edward Brown baadaye aliiambia mahakama kwamba kwamba ndege ya kwanza ingeondoka Julai 24.
Kuzuia wanaotafuta hifadhi
Mpango huo - uliotayarishwa kwa mara ya kwanza na mmoja wa watangulizi wa Sunak, Boris Johnson, mwaka wa 2022 - unalenga kuwazuia wanaotafuta hifadhi kufanya safari hatari kuvuka kwa boti ndogo kutoka Ufaransa.
Novemba mwaka jana, Mahakama ya Juu ya Uingereza ilitangaza sera hiyo kuwa ni kinyume cha sheria, jambo lililosababisha Sunak kutia saini mkataba mpya na nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kupitisha sheria mpya ya kubatilisha hili.
Wakili wa Shirika la Asylum Aid Charlotte Kilroy alisema tarehe iliyopangwa kwa ndege hiyo ni "habari kwetu," Jaji, Martin Chamberlain, alisema.