Bunge la Uganda limefanya programu maalum ya kumuomboleza Mkuu wa shirika la Usalama wa Ndani (ISO) Charles Oluka aliyefariki 29 Januari 2024.
"Charles hakuwa tu rafiki wa kibinafsi lakini pia mzalendo aliyejitolea ambaye alitumikia nchi yake kwa kujitolea. Hakika kifo chake ni kinaskitisha kubwa," Anita Among, Spika wa bunge la Uganda alisema.
Naibu Spika, Thomas Tayebwa naye ameliongoza Bunge katika kumuenzi mwanajeshi huyo akisema katika kipindi chake cha uongozi, alifanya kazi kubwa ya kuimarisha sura ya Shirika la Usalama wa Ndani ambalo limekuwa likikosolewa na wananchi hapo awali kwa utovu wa usalama, wakidai ya kwamba lilihusika katika utekaji nyara wa Waganda, kuwatesa na kuwaweka kizuizini kinyume na sheria.
“Ni mtu muungwana ambaye ametumikia nchi hii kwa bidii. Mambo mengi mazuri yalikuwa yameanza kutokea katika maisha yake, alifunga ndoa mwaka jana, alikuwa ametoka tu kupandishwa cheo. Alikuwa na maisha ya furaha," Tayebwa alisema katika kikao cha bunge.
"Na nadhani alikuwa ameleta taswira bora ya Shirika la Usalama wa Ndani, sio ISO ya zamani ambapo tungekuwa na masuala siku hadi siku. Nadhani taswira ya shirika hilo chini yake limeimarika sana," Naibu spika aliongezea.
Oluka alipandishwa cheo Januari 2024 kuwa Brigedia Jenerali na Rais Yoweri Museveni, amefariki akiwa na umri wa miaka 54.
Afisa wa mawasiliano wa Rais alisema kuwa Brigedia Jenerali Charles Oluka alifariki katika hospitali ya Seguku jijini Kampala tarehe 29 Januari 2025.