Waendesha mashitaka nchini Uganda wamemshtaki kamanda wa wanamgambo wanaoshukiwa kuhusika mauaji ya watalii wawili wa kigeni na dereva wao mwezi uliopita.
Kamanda wa wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF), Abdul Rashid Kyoto, maarufu Njovu, alikamatwa mapema mwezi huu, na pia anatuhumiwa kuongoza mauaji ya kuogofya katika shule moja mwezi Juni.
Vile vile, Uganda pia imeilaumu ADF, ambayo inashirikiana na Kundi la Daesh, kwa mauaji ya watalii waliokuwa fungate na mwelekezi wao wa ndani, pamoja na shambulio la shule ambalo lilisababisha mauaji ya watu 42, wengi wao wakiwa wanafunzi.
Waendesha mashtaka "wameidhinisha mashtaka mawili ya ugaidi, mashtaka matatu ya mauaji, mashtaka matatu ya wizi uliozidishwa na mashtaka moja ya kuwa mali ya shirika la kigaidi" juu ya shambulio la watalii, mkurugenzi wa mashtaka ya umma alisema katika taarifa Jumatatu.
Kundi la Daesh, lilitangaza kuhusika mauaji hayo, likisema kuwa liliua "watalii watatu Wakristo".
Waendesha mashtaka walisema Njovu alikamatwa katika ziwa Edward, linalozunguka mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nao washirika wake wawili waliuawa kwa kupigwa risasi wakati "wengine walifanikiwa kutoroka kwa mashua na silaha zao".
Hapo awali, jeshi lilisema kuwa Njovu pekee ndiye aliyeponea kwenye operesheni hiyo.
Kundi la ADF ndilo kundi baya zaidi kati ya makundi kadhaa yenye silaha ambayo yanasumbua mashariki mwa Kongo, huku likishutumiwa kwa kuwaua maelfu ya raia huko, na pia kufanya mashambulizi ya kuvuka mpaka.
Baada ya shambulio la mwezi Oktoba, Rais Yoweri Museveni alitoa wito kwa vikosi vya usalama kuhakikisha ADF "ilifutwa" na jeshi limefanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya makao yake nchini DRC.