Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR linasema idadi ya wakimbizi nchini Uganda inakaribia kufikia milioni mbili.
Kwa sasa takwimu zinaonyesha kuwa Uganda ina wakimbizi 1,702,278.
"Hofu yetu ni kuwa huku idadi ikiongezeka kila siku rasilimali tunazozipata zinapungua. Je, Uganda ikifunga milango yake na kusema rasilimali zimepungua na hatutataki tena wakimbizi, hiyo si itakuwa changamoto?" amesema Lilian Abera Waziri wa nchi wa Wakimbizi.
Kufikia mwishoni mwa Juni 2024, takwimu za UNHCR zinaonyesha Uganda ilikuwa ikipokea wakimbizi 1,702,278 na wanaotafuta hifadhi. Wageni wapya waliendelea kuingia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan na Sudan Kusini.
UNHCR inasema mahitaji ya wakimbizi mwaka 2024 ni dola milioni $343.4 lakini kufikia Juni 2024 ni dola milioni 81.1 peke yake ndiyo ilikuwa imepokelewa.
Serikali imeonyesha hofu kuwa upungufu wa fedha za kuwasaidia wakimbizi hawa huku kipaumbele cha jamii ya kimataifa kikielekezwa katika vita kati ya Urusi na Ukraine, na maeneo ya Israel na Palestina.
"Hali ya wakimbizi hapa nchini Uganda ni suala la jamii ya kimataifa kulichukulia kwa uzito, hivyo jamii ya kimataifa lazima iisaidie Uganda," Charles Odongtho msemaji katika ofisi ya Waziri Mkuu amesema.
Wakimbizi nchini uganda wanaishi katika wilaya 12 nchini humo huku Uganda ikiwa na sera ya mlango wazi. Hii inamaanisha kuwa wakimbizi wanakaribishwa nchini, wanapewa ardhi na huduma za msingi.
Wanafurahia uhuru wa kutembea ingawa hawapewi uraia wa Uganda.
Tangu mwanzo wa mwaka, UNHCR inasema Uganda imepokea 69,605 wakimbizi hasa kutoka Sudan (26,796), Sudan Kusini (14,031), Eritrea (11,520), na DRC (14,280).
Kuongezeka kwa wimbi la wakimbizi kumesababisha msongamano wa watu katika baadhi ya maeneo wanayokaa kwa muda kabla ya kupelekwa katika maeneo mengine ya makazi.