Uganda inatumia zaidi ya dola milioni 524 kila mwaka kwa huduma za kudhibiti Ukimwi, takriban zaidi ya dola milioni 271 ikitolewa kwa matibabu na ufuatiliaji wa maabara. / Picha: Reuters

Tume ya Kudhibiti UKIMWI Uganda (UAC) imetoa wito kwa Bunge na Wizara ya Fedha kufanya mabadiliko katika vipaumbele vya bajeti ya nchi hiyo na kutenga zaidi ya dola milioni 81.3 (Shilingi bilioni 300) za ziada ili kukabiliana na pengo la ufadhili lililoachwa na uamuzi wa serikali ya Marekani kusitisha misaada kutoka nje.

Hii inafuatia amri ya utendaji iliyotiwa saini na Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha misaada kwa baadhi ya miradi.

Wito huo ulitolewa na Dkt. Vincent Bagambe, Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati katika UAC, ambaye alifika mbele ya Kamati ya Afya ya Bunge mnamo Februari 11, 2025.

Katika taarifa yake mbele ya kamati, alisisitiza haja ya dharura ya kuongezeka kwa mgao wa bajeti, haswa kwa bidhaa muhimu.

“Tunalishauri bunge kuangalia upya vipaumbele vya bajeti na kuongeza fedha kwa ajili ya huduma za kudhibiti ukimwi kwa kuongeza zaidi ya dola milioni 81.3 (Shilingi bilioni 300) ili kugharamia dawa, vifaa vya maabara na rasilimali nyingine zilizotolewa na PEPFAR," Bagambe alisema.

" Hii inatakiwa kuwa pamoja na nyongeza za kila mwaka za zaidi ya dola milioni 13.5 (Shilingi bilioni 50) katika usaidizi wa bajeti. Lengo letu la muda mrefu ni kugharamia kikamilifu dawa za kurefusha maisha (ARV) na gharama nyingine za bidhaa, kuruhusu washirika kuzingatia kujenga uwezo wao wa usaidizi wa kijamii, na usaidizi wa kiufundi,” Dkt. Bagambe alisema.

Hali ya maambukizi ya ukimwi Uganda

Hadi kufikia Disemba 2023, idadi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini Uganda ilikuwa milioni 1.492, huku wanawake wakiwa 910,000, wanaume 520,000 na watoto 72,000 wakiathirika.

Katika kipindi hicho, Uganda kulikuwa na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi 38,000, kati yao 22,000 ni wanawake, 11,000 wanaume, na watoto 4,700.

Zaidi ya hayo, kulikuwa na vifo 20,000 vilivyotokana na ukimwi, huku wanawake wakiwa 8,200, wanaume 8,400, na watoto 3,200 .

Wabunge walifahamishwa kuwa Uganda inatumia zaidi ya dola milioni 524 (trilioni 1.928) kila mwaka kwa huduma za kudhibiti virusi hivyo huku 60% ambayo ni takriban dola milioni 271(trilioni 1) ikitolewa kwa matibabu na vipimo vya maabara.

Kati ya fedha hizo, serikali ya Uganda inachangia zaidi ya dola milioni 62 (bilioni 230), huku wafadhili wa kimataifa wakitoa kiwango kilichobaki, hasa serikali ya Marekani na Mfuko wa Kimataifa.

PEPFAR pekee inachangia takriban zaidi ya dola 92.4(shilingi bilioni 340) kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya afya, ikijumuisha mishahara kwa wahudumu wa kliniki 4,333 na wahudumu wa afya wa jamii 26,690.

TRT Afrika