Katika kikao cha ufunguzi rasmi wa mkutano wa Muungano wa Nchi Zisizofungamana upande wowote, (Non aligned Movement, NAM) unaoendelea mjini Kampala, Uganda, Rais Yoweri Museveni alichaguliwa kwa kauli moja kuwa mwenyekiti wa NAM.
"Nguvu ya NAM inapaswa kutumika kuwa na ushawishi mkubwa, haswa katika UN, katika mchakato mzuri wa kuleta mabadiliko kwa mustakabali bora wa pamoja," Rais Museveni wa Uganda alisema.
Uganda, ambayo imechukua hatamu kutoka Azerbaijan, itahudumu kwa miaka mitatu katika Jumuia hiyo iliyoanzishwa mwaka 1961.
Mkutano huo umekashifu kile ambacho wanachama wameita unyanyasaji kutoka kwa nchi nyengine.
"Wanyanyasaji wa rangi, dini, kabila au jinsia, wanapaswa kuacha kupoteza muda na fursa zetu, na mipango yao ya kina," Museveni amesema.
Museveni ameuhakikishia ujumbe wa NAM kwamba picha zinazoonyesha uhaba wa chakula barani Afrika mtandaoni zinapaswa kupuuzwa.
Amesisitiza kuwa Afŕika ina rasilimali ya kutosha ya chakula, na kuitaka dunia kutupilia mbali simulizi za kupotosha.
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ameuambia mkutano huo kuwa vita Gaza ni lazima visitishwe.
"Afrika inalaani kanuni hii isiyokubalika ya kimaadili na kushindwa kwa kibinadamu na inadai kukomeshwa mara moja kwa vita dhidi ya watu wa Palestina na kwa utekelezaji wa haraka wa suluhisho ya mataifa hayo mawili, " Faki amesema.
Nayo Ethiopia imepaza sauti yake kuhusu changamoto ya nchi zisizo na bahari.
"Nchi zisizo na bahari zinakabiliwa na changamoto kubwa zinazozuia uwezo wao wa kutimiza matakwa ya watu wao ya kupata riziki ya kutosha na endelevu na kuhakikisha maendeleo yao," Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema.
"Ethiopia inaendelea kutafuta suluhu ya amani na yenye manufaa na mazungumzo kwa changamoto hiyo," amesema.
NAM ilianzishwa 1961 ikiwa na nia ya kuanza njia huru katika siasa za ulimwengu ambayo ingefanya nchi wanachama wasiwe waathiriwa katika mapambano kati ya mataifa yenye nguvu zaidi.
Sudan Kusini inatarajiwa kuingizwa katika kundi hili la wanachama 120.