Rais Museveni anasema licha ya changamoto za ndani ya nchi na kimataifa Uganda inaendelea kiuchumi / Picha kutoka Ikulu Uganda  

Miaka 38 iliyopita, siku kama ya leo, Rais wa sasa nchi hiyo aliliongoza jesho la National Resistance Army kumuondoa madarakani Tito Okello Lutwa, aliyekuwa kiongozi wa awamu ya nane wa Uganda.

Katika miongo mitatu ya utawala wake, Rais Museveni ameshuhudia Uganda ikipiga hatua kwenye nyanja tofauti, zikiwemo za kijamii, kisiasa na uchumi.

" Ushindi wa NRM wa tarehe 26 Januari, 1986, ulikuwa ni kiashiria cha uimara wa watu wetu na uwezo wao wa kukabiliana na changamoto mbalimbali," anasema Museveni katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa siku ya Alhamisi.

Kiongozi huyo mwenye bashasha nyingi ana amini kuwa Uganda inaendelea kuwa imara katika kukabiliana na changamoto kadha wa kadha.

Usalama ni mojawapo ya changamoto hizo , hasa za mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kikundi kwa kikundi cha ADF.

Mwaka uliopita waasi hao waliripotiwa kuwashambulia na kuwaua watalli kutoka Uingereza na Afrika Kusini, akiwemo dereva wao mwenye asili ya Uganda.

"Usalama wa nchi unaendelea kuwa imara na Serikali inaboresha zaidi uwezo wake wa kiusalama na miundombinu ya kisasa ili kugundua matukio ya kigaidi kabla hayajatokea," Museveni anasema.

Kiongozi huyo anasisitiza kuwa Uganda imeboresha na kuongeza uwezo wake wa kupeleleza na kufuatilia viashiria vya matukio hatarishi ili kuhakikisha kwamba Waganda na watu wengine wanaendelea kubaki salama.

" Usalama wa nchi unaendelea kuwa imara na serikali inaboresha zaidi uwezo wake wa usalama na miundombinu ya kisasa ili kutambua matukio ya kigaidi kabla hayajatokea. Tumeboresha sana uwezo wetu wa upelelezi na ufuatiliaji ili kuhakikisha kwamba Waganda na wageni wetu wanaokuja hapa wako salama," Museveni anaongeza.

Ukuaji wa Uchumi

Museveni amewahakikishia wananchi wake kuwa uchumi wa nchi yao unaendelea kukua licha ya changamoto kama athari za mabadiliko ya tabia nchi kwenye kilimo na miundombinu kutokana na mafuriko.

Changamoto zingine ni mzozo unaoendelea Ulaya Mashariki, ambao umesababisha bei ya bidhaa muhimu kama vile mafuta kupanda katika siku za hivi karibuni.

" Uchumi wetu ulikua hadi kufikia dola za Kimarekani bilioni 49.5 katika mwaka wa fedha 2022/2023, kutoka dola bilioni 45.6 zilizopatikana mwaka wa fedha 2021/22," anafafanua.

Kwa sasa, Uganda inatazamia kupata maendeleo zaidi ya kiuchumi, kwa miaka ijayo.

" Uchumi utakua kutoka thamani yake ya sasa ya dola za Kimarekani bilioni 48 kwa mwaka wa fedha 2022/23 hadi dola bilioni 55 kufikia mwisho wa mwaka wa fedha huo na kwenda mbali zaidi kufikia dola bilioni 60 katika mwaka wa fedha 2024/25," anasema Rais Museveni.

Uhusiano na DRC

Nchi hiyo pia inapanga kuwa jirani mwema kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

" Ili kupanua biashara ya kikanda na kusaidia maendeleo ya kikanda, Uganda inafanya miradi ya pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kutekeleza mbinu za kupunguza gharama za usafirishaji, na kuboresha miundombinu ya mpaka ili kuwezesha biashara na huduma za kifedha katika eneo lote," anaeleza.

Miradi hiyo, kwa mujibu wa Rais Museveni itaangazia barabara na sekta ya nishati kwa nchi hizo mbili.

Uganda inalenga soko hili kwa ajili ya kuongeza mauzo yake ya nje na kutoa nafasi zaidi za ajira kwa wananchi wake.

TRT Afrika