Uganda imeamua kuweka Mamlaka ya Maendeleo ya Kahawa Uganda (UCDA) na Mamlaka ya Maendeleo ya Maziwa (DDA) kuwa chini ya Wizara ya Kilimo.
Hii ni baada ya Rais Yoweri Museveni kukutana na baadhi ya Wabunge wa Kamati za Bunge za Kilimo, Uchumi wa Kitaifa na Fedha.
Hii itachukua muda wa miaka mitatu.
“Kwa hiyo uamuzi ni kwamba tuna miaka mitatu ya UCDA, kwenda mbele, ili mwisho wa miaka mitatu, wadau wote wawe wamefikia hitimisho la jinsi ya kushughulikia sekta ya kimkakati ya kahawa," Bataringaya, mbunge wa Kashari Kaskazini aliwaeleza wandishi wa habari.
"Ina maana kwamba UCDA itaendelea na udhibiti wa sekta ya kahawa, lakini ikisaidiwa na Wizara ya Kilimo kwa sababu hofu ya Wabunge ni kwamba huenda wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo hawana uwezo ambao umejengwa ndani ya UCDA wa kuendesha sekta yetu ya kahawa,” Bataringaya aliongezea.
Wabunge wengine wamepinga.
"Tulimwambia Rais kwamba Wizara, ambapo anataka kupeleka Mamlaka ya Kahawa haijaonyesha ufanisi. Wizara ya Kilimo ina mikopo mingi ya mamilioni ya dola ambayo wameshindwa kulipa. Wanatembea kila mahali ulimwenguni. Kwa hiyo, tukamwambia kwamba hatuwezi kuchukua bidhaa hii ya kimkakati na kuikabidhi Wizara, ” Abed Bwanika mbunge wa Kimaanya-Kabonero amesema.
Wabunge wengine walielezea hofu yao kuhusu hatari ya sekta ya kahawa ya Uganda kuathiriwa, ikiwa kutakuwa na ulegevu katika udhibiti wake wakati ikiwa chini ya Wizara ya Kilimo.
"Na hofu yetu ni kwamba sekta ambayo imeshika kasi haipaswi kupotezwa. Tusipoteze mwelekeo na mifuko milioni 20 tunayotarajia kwa muda mfupi inapaswa kuwa lengo ambalo tutafikia," ameongeza Bataringaya.
"Changamoto ni kwamba sheria inaundwa lakini utekelezaji unawekwa utakuja baadae," amesema.
Mwaka 2023/24, mauzo ya kahawa nje ya nchi yalikuwa ni magunia milioni 6.13 yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1.144 .
Mamlaka ya kahawa ya Uganda ilikuwa na mpango wa kuweka mikakati mengine kuongeza uzalishaji, lakini sasa itabidi isubiri mipango ya Wizara.