Serikali ya Uganda imekubali kujadili upya ruzuku ya Dola za Marekani milioni 217 (Shs796,476,800,000) kutoka Benki ya Dunia iliyokusudiwa kuwasaidia wajasiriamali wanawake nchini Uganda.
Hii ni baada ya wabunge kuibua wasiwasi juu ya mgao mdogo wa Dola milioni 35 pekee (Sh.128,464,000,000) ambazo zitanufaisha moja kwa moja wanawake, wakati nyengine zitakwenda kwenye mafunzo na kusimamia mfuko huo.
"Tunawashukuru kwa kutoa hoja hii lakini pia tumezingatia kama Wizara ya Jinsia majadiliano kati ya serikali na Benki. Bila shaka, tuko hapa kwa madhumuni kwamba raia wa Uganda ndiye ambaye anafaa kufaidika na mradi huo,” alisema Esther Anyakun, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Kazi.
Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Henry Musasizi, alifanya kikao cha saa 6 kilichofanyika kati ya Kamati ya Hesabu za Serikali, sambamba na maofisa wa Wizara ya Jinsia na Taasisi ya Sekta Binafsi Uganda, ambavyo ni vyombo viwili vinavyosimamia mfuko huo.
"Tunazingatia wasiwasi wako kwamba munataka wanaolengwa wanufaike zaidi, kupata kiasi kikubwa, meneja yeyote mwenye busara angetaka hili litendeke . Tuna utaratibu wa kushirikiana na Benki, nataka kuahidi kwamba tutashirikiana na Benki kwa nia ya kuzingatia, baadhi ya masuala haya munayoyaibua," Musasizi ameiambia kamati ya bunge.
"Najua ndani ya kipengele, inawezekana kuhamisha fedha kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa hivyo, tutashirikiana na Benki ya Dunia kwa nia ya kutimiza maombi haya,” alisema Waziri Musasizi.