Rais Yoweri Museveni ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa ajili ya sensa ya kitaifa ambayo inatarajiwa kuanza leo.
" Tunapoelekea kufikia dira ya Uganda 2040 ya maendeleo, ni muhimu tupange kwa kuzingatia rekodi sahihi kuhusu watu na rasilimali zetu," Rais Museveni amesema.
Kila baada ya miaka 10, Uganda hufanya sensa ya kitaifa, takwimu ya mwisho ilifanyika mwaka wa 2014.
" Tafadhali jitokeze na uwape wakusanyaji data au wadadisi wetu majibu ya uaminifu kwa maswali yao, ili kuwawezesha kupata maelezo sahihi zaidi kukuhusu wewe, kaya zako na jamii," rais Museveni ameongezea katika ujumbe wake kwa taifa.
Watu wataanza kuhesabiwa usiku wa 9 Mei, 2024.
" Serikali ilikubali kuteua tarehe 9 Mei, 2024 kuwa ni usiku wa sensa. Wale wote watakaolala Uganda watahesabiwa," Chris Baryomunsi waziri wa mawasiliano amesema.
" Senya yenyewe ya taifa itaanza tarehe 10 Mei, 2024, saa sita kamili usiku, Nawaomba sote tujikumbushe, siku hiyo itatangazwa siku ya mapumziko ili waandikishaji wawakute nyumbani.” Baryomunsi ameongezea.
Popote mtu atakapojipata saa sita za usiku ndipo kutatumika kama eneo lake la kuhesabiwa.
Takwimu za sensa zina umuhimu katika kuongoza mipango, uundaji wa sera, na utekelezaji wa programu tofauti nchini. Pia data inayopatikana inasaidia kufuatilia maendeleo kulingana na malengo ya kitaifa.
" Wanafunzi katika vyuo vikuu watahesabiwa kwenye kumbi zao za makazi, " Chris Mukiza , kamishna wa sensa ameelezea.
" Hakuna sehemu ambayo hatutafikia ikiwa ni pamoja na magereza au makambi ya majeshi. Wote watahesabiwa," Mukiza amesema.
Ofisi ya takwimu ya Uganda imeahidi kuheshimu data ya sensa.
" Ningependa kuwahakikishia umma kwa ujumla kwamba maelezo yote yatakayokusanywa wakati wa zoezi yatakuwa siri na kutumika tu kama data ya kujua jumla ya watu na makazi," Amos Lugoloobi waziri wa fedha wa Uganda amesema.
Kulingana na Ofisi ya takwimu ya Uganda, UBOS, idadi ya watu nchini Uganda kwa sasa ni takriban watu milioni 45.5 , huku ukuaji ukiangaliawa kuwa asili mia 30.4.
Sensa hii imepangwa kufanyika kwa siku 10.